AZAM FC YAICHAKAZA AFRICAN LYON

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki, Azam FC, imefanikiwa kuichapa African Lyon mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jana usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulioathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia asubuhi, ulikuwa ni maalum kwa ajili ya benchi la ufundi la Azam FC kukipima kikosi chake na kuwaweka wachezaji kwenye ushindani kutokana na kutokuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) wikiendi hii.
Mabao pekee ya Azam FC yameweka kimiani kiufundi na beki wa kulia, Erasto Nyoni, dakika ya 23 aliyefunga bao lake la pili kwenye mechi ya pili mfululizo, jingine akifunga katika ligi wiki iliyopita timu hiyo ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Ruvu.
Bao jingine la mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu usiku huu lilifungwa na kiungo Mudathir Yahya, dakika ya 87 aliyemalizia kazi nzuri na winga Enock Atta Agyei, ambaye ni mmoja wa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Azam FC Aristica Cioaba, alipata fursa ya kuwatumia kwa mara ya kwanza wachezaji wake watatu waliokuwa majeruhi, mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed na kiungo Stephan Kingue, ambao aliwachezesha kwa dakika 55 kabla ya kuwafanyia mabadiliko.
Pia aliwajumuisha kikosini wachezaji wanne wa timu ya vijana ya Azam FC, mabeki Abbas Kapombe, Said Mohamed, pamoja na kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaidi, ambao wawili hao walicheza dakika saba za mwisho.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC leo hii kitakuwa na mapumziko kabla ya Jumatatu kuanza mandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika wikiendi ijayo huku timu itakayopangiwa nayo ikitarajia kujulikana leo hii

No comments