NGORONGORO HEROES KUPAA KESHO KUWAFUATA DR CONGO,MAMLAKA YA HIFADHI YATOA UDHAMINI

Na Said Ally
Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana Ngorongoro Heroes kinataraji kusafiri kesho alfajiri kuelekea nchini DR Congo kwa ajili ya ushiriki wa mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 20.

Afisa Habari wa TFF,Clford Mario Ndimbo amesema kwamba safari hiyo ya Ngorongoro Heroes imechagizwa na udhamini wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro Heroes ambao wao wametoa udhamini wa usafirishaji wa timu hiyo ya vijana.

Alisema kwamba kikosi kinataraji kusafiri na wachezaji 21 kwa ajili ya mchezo huo ambao Ngorongoro Heroes itawalazimu kupata ushindi ili au sale ya magoli ifanikiwe kusonga mbele kwenye michuano hiyo baada ya mechi ya awali iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam timu hizo kutoshana nguvu kwa kutoka sale ya ya bila kufungana.

Nae kaimu meneja wa uhusiano mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Joyce Mgaya alisema kwamba wameamua kutoa udhamini huo kwa timu ya vijana baada ya kutambua umuhimu wa timu hiyo ambayo imebeba jina la Hifadhi hiyo.

Alisema kwamba kwa upande wao wataendelea kutoa udhamini kwa timu hiyo kwani wamebaini kupitia wao wana nafasi kubwa ya kutangaza Hifadhi hiyo katika nchi tofauti kutokana na ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali ya vijana.

Kwa upande wake kocha mkuu wa timu ya Ngorongoro Heroes Ammy Ninje alisema kwamba kwa upande wa maandalizi kila kitu kipo vizuri kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Dr Congo.

Aliongeza kwa kusema kwamba kwa sasa ameshayanyia kazi mapungufu ambayo yalionekana katika mchezo uliopita hivyo matumaini kwa vijana wake kusonga mbele kwenye mashindano hayo ni makubwa.

Nae nahodha wa Ngorongoro Heroes,Issa Abdi Makame kwa upande wake ameishuruku mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kujikita kutoa udhamini kwa timu hiyo akiamini kuwa kuelekea kwenye mchezo wao dhidi ya DR Congo watafanya vizuri.

Ngorongoro Heroes inataraji kushuka dimbani siku ya jumapili ya tarehe 21 huko Dr Congo kumenyana na wenyeji wao,mchezo ambao utaamua mshindi atakaesonga mbele kwenye mashindano hayo ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika.

No comments