MWENYEKITI WA MASHINDANO YANGA ATOA NENO KUELEKEA MECHI YA SIMBA

Na Said Ally
Mwenyekiti wa mashindano  ndani ya klabu ya Yanga,Hussein Nyika amesema kwamba mechi yao dhidi ya Simba inayotarajiwa kupigwa April 29 mwaka huu haimpi presha yoyote.

Nyika alisema kwamba Simba ni timu ya kawaida hivyo hawawezi kuweka mkazo zaidi katika mechi hiyo kwani hata wasipofanya maandalizi kwa wakati huu  bado wana nafasi ya kuifunga.

Alisema kwamba kutokana na ubora wa kikosi chao na uzoefu ambao wameupata kupitia michuano ya kimataifa ana imani Yanga itachomoza na ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Aidha katika hatua nyingine Nyika alisema kwamba kwa sasa wanasubiri kupata mapendekezo kutoka kwa benchi la ufundi ili kuanza mchakato wa kusajili wachezaji ambao watawaongeza kwa ajili ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Kwa mujibu wa kanuni za CAF Yanga ina nafasi tatu za kusajili wachezaji kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwenye michuano hiyo ya kimataifa baada ya kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi.

No comments