SIMBA WATAKIWA KUJIONGEZA,VINGINEVYO KOMBE WATALIPATA NDOTONI

Na Joseph Msami, New York

Niliwahi kuandika makala baada ya mchezo wa ngao ya jamii, ambayo ilieleza namna hamasa ilivyoisadia Simba kushinda nje ya uwanja na kisha wakamalizia kwa mikwaju 4 ya panalti dhidi ya 3 ya mahasimu wao Yanga.
Nimeanza hivyo kwa kuwa wana Msimbazi hao kama ilivyokuwa katika mchezo huo, walikuwa na hamasa kubwa ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, mchezo ambao hata hivyo umetoa taswira tofauti na wengi walivyowachukulia poa wana Jangwani, Yanga.

Matarajo ya ushindi yalipitiza.
Mashabiki wa Simba walio wengi waliamini kuwa wana asilimia zaidi ya 90 za ushindi katika mchezo wa jumamosi. Wengi walithubutu hata kuwakejeli Yanga kuwa watawafunga idada kubwa ya magoli. Ni kawaida kwa mashabiki kuzodoana kabla, wakati na baada ya mchezo, lakini kama ilivyokuwa katika mchezo wa ngao ya jamii, iliwalazimu Simba kusubiri hadi matuta ili  kushinda.

Katika mchezo wa jumamosi ambao Simba waliduwazwa na ushindani wa Yanga na kumaliza kwa droo ya moja moja, sababu za kujiamini Simba kama ilivyokuwa hapo awali, zilitokana na wachezaji wakonge waliosajiliwa msimu huu kwa gharama kubwa kama vile Emmanuel Okwi, Hruna Niyonzima, John Bocco na golikipa namba moja Tanzania, Aish Manula. Haina ubishi kwamba wachezaji hawa ni wazuri na wazoefu.

Kukosekana kwa wachezaji tegemeo wa Yanga waliokuwa majeruhi akiwamo kiungo Thabani Kamusoko, mshambuliaji mwiba wa Simba Amiss Tambwe, na Donald Ngoma, kulinogeza ushindi hamasa na matarajio ya Simba.

Yanga walijipanga.
Ukiangalia takwimu za mchezo,ni wazi kuwa Simba walitawala mchezo zaidi. Lakini Yanga ndio waliofanya mashambulizi hatari zaidi langoni mwa Simba yaani (shoots on target). Ikiwa mashabiki wa Simba walitaka kufurahia chenga twawala basi walifarijika, lakini siamini kwamba Simba ambao wamukosa ubingwa kwa muda mrefu, wanataka kufuarhia kumiliki mpira pekee, wanahiyaji ushindi ili kuchukua kombe la ligi kuu.

Yanga walimakinika, wakijua hawana wachezaji tegemezi. Mathalani upande wa kiungo, vijana chipkizi kama Gadiel Michael walihakikisha wanalidhibiti dimba, huku wakichagizwa na uchezaji wa kipekee wa kiungo mkabaji Papy Kabamba ambaye alimpa wakati mgumu Aish Manula kwa mikwaju ya hatari.

Kocha Lwandamila shujaa.
 Bila shaka umaarufu wa kocha wa Yanga Geroge Kwandamina ‘‘chicken” umeongezeka baada ya mchezo na watani wao wa jadi Jumamosi Oktoba 28,2017. Sababu kubwa na ambayo pengine waweza kuibaini ukiwa mwanamichezo (sio shabiki pekee), ni namna alivyokiandaa kikosi kupambana na Goliati na akawapa mbinu za namna wanavyoweza kuzuia huku wakishambulia na kufanikiwa kuwadhibiti Simba ambao walitumia muda mwingi kupiga pasi ambazo hazikutengezeza nafasi toshelevu kupata ushindi.

Ikumbukwe kocha huyu na kikosi ambacho wachezaji wengi wa msimu uliopita hawapo. Wachezaji kama kipa Deogratuis Mushi na Simon Msuva ambao wanacheza soka la kulipwa, Deo Kaseke aliyenunuliwa na Singida United  na wengine ambao hawamo kikosini kwa sababu kadhaa.

Ndio mana katika hili naungana na mwanamichezo Baraka Mbolembole kwamba kocha huyu anaweza na haitashangaza, akiipa Yanga ubingwa mwaka huu.

Simba ikomae
Baada ya mchezo huo, morali na kujiamini kwa Yanga,ambayo inaripotiwa kukabiliwa na UFEMI (Ukosefu wa Fedha Mifukoni), itaongezeka na pengine ikaendeleza wimbi la ushindi hasa pale majeruhi watakaporejea.
Simba wanapaswa kufahamu sasa kwamba haitakuwa rahisi kwao, na wasisubiri muujiza, kwani hata muujiza unahitaji Imani ambayo ni gharama kubwa. Inapaswa kujitutumua, ili kudhihirisha kuwa mabilioni ya fedha za usajili, na neema ya  KUFEMI (Kujawa na Fedha Mifukoni) vyaweza kuleta mabadiliko.

Ikiwa hawatatwaa kombe mwaka huu, itakuwa ngumu sana kukitumia kikosi hicho kwa mwaka ujao kupata ushindi , licha ya hoja kwamba kwamba wanahitaji muda waelewane . Kuna uwezekano mkubwa watacheza wakikabiliwa na shinikizo kubwa la mashabiki wenye njaa na vikombe jambo linaloweza pia kuleta mgogoro ndani ya klabu hiyo.

Joeph Msami ni mwanamcihezo ambaye kwa sasa yuko kikazi mjini New York, Marekani. Waweza kumpatia maoni kupitia +1 646 546 4122.

No comments