AZAM FC YAISOGEZA YANGA KWENYE MSIMAMO WA LIGI

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Azam FC imekaa kileleni baada ya kufikisha jumla ya ponti 19 ilizozipata baada ya kushinda mechi tano na kutoka sare nne, huku ikiwa ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache hadi sasa ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu katika mechi tisa ilizocheza hadi sasa.
Baada ya kosakosa nyingi na upinzani mkubwa iliyoupata kwa Ruvu Shooting, hatimaye Azam FC ilijipatia bao hilo pekee kwenye dakika mbili za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika likifungwa kiustadi na mshambuliaji Yahya Zayd kiaunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha msaidizi Aggrey Moris.
Hilo ni bao la kwanza Zayd kufunga msimu huu na bao la saba kwa timu hiyo kufunga kwenye msimu huu wa ligi, asilimia 90 ya mabao hayo yakifungwa na Mbaraka Yusuph, aliyetupia nyavuni matatu mpaka sasa.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupoumzika kwa siku mbili kabla ya kuanza tena mazoezi Jumanne ijayo ikijiandaa na mchezo ujao wa ligi utakaofanyika wiki mbili zijazo dhidi ya Njombe Mji ukipigwa Novemba 18 mwaka huu katika Uwanja wa Sabasaba, mkoani Njombe.
Mechi za ligi hazitakuwepo wiki ijayo kutokana na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambapo Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kucheza mchezo wana Benin ugenini utakaofanyika wikiendi ijayo.

No comments