SPORTPESA YALETA KUFURU KWENYE UDHAMINI WA SIMBA

Timu ya soka ya Simba imeikaribisha kwa stahili ya aina yake kampuni mpya ya SportPesa ambayo leo hii kwa mara ya kwanza hapa nchini imetoa udhamini mnono wa shilingi bilioni 4.9kwa klabu hiyo yenye makazi yake mitaa ya Msimbazi jijini Dar es salaam.

Simba imeingia udhamini huo kwa muda wa miaka mitano ambapo leo hii wakati wa mechi yao ya ligi kuu ya Tanzania bara dhidi ya Stend United iliyoisha kwa wekundu hao kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 walioneka na jezi zenye nembo ya kampuni hiyo iliyojikita kwenye michezo wakati wa kipindi cha pili.

Mkataba huo mnono ambao ni wa kwanza kutokea ndani ya klabu ya Simba utaifanya Simba ijinyakulie kitita cha shilingi milioni 888 katika mwaka wa kwanza na pia itapewa shilingi bilioni moja na milioni 80 katika mwaka wa mwisho wa mkataba kwa kuwa kila mwaka,asilimia 5 ya fedha inaongezeka.

Aidha klabu hiyo itapewa shilingi milioni 100 endapo wekundu hao wa Msimbazi watachukua ubingwa ikiwa kama motisha kutoka kwa SportPesa na pia watapewa shilingi milioni 250 wakichukua kombe la Kagame au michuano inayoandaliwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Hata hivyo unaweza kusema kwamba kama klabu hiyo imeanza kwa neema katika udhamini huo kwani katika mechi ya kwanza timu ikiwa chini ya udhamini wa SportPesa imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stend United katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa.


No comments