BARAZA LA TAIFA LA MICHEZO ZANZIBAR LATOA SIKU 30 KWA VYAMA VYA MICHEZO KUFANYA UCHAGUZI
Na Sleiman Ussi Zanzibar .
BARAZA la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), limeviagiza vyama vya michezo ambavyo havijafanya uchaguzi kufanya hivyo ili kupata viongozi kulingana na katiba zao na waziagize klabu zao kufanya uchaguzi ili waongoze kwa demokrasia na kwa kufuata katiba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa BTMZ, Khamis Ali Mzee , iliyotolewa jana Afisini kwao Mwanakwerekwe, baraza hilo limetoa mwezi mmoja (siku 30) kuanzia jana 16/5/2017 hadi 16/6/2017 ili kila chama na klabu kutekeleza maelekezo hayo.
“Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar kupitia Afisi yetu ya Mrajis wa Vyama vya Michezo na Vilabu tumegunduwa kuwa kuna vyama vya michezo Taifa vimeshamaliza muda wao na bado vinaendelea kuwepo madarakani, sisi kama Baraza hatukubaliani na baadhi ya Viongozi wa Vyama kujisahaulisha kufanya uchaguzi, sasa tayari tushaweka wazi na kuna orodha ya vyama 5 vitaanza zoezi hilo”. Alisema Mzee.
Nae Mrajisi wa vyama vya michezo vya Zanzibar Suleiman Pandu Kweleza amesisitiza vilabu kufuata kanuni na katiba ziilizowekwa kuanzia jana hadi kufika tarehe 16-6- 2017 wawe wameshafanya uchaguzi na kupata viongozi wapya.
“Afisi yangu kuna vyama zaidi ya 33, kuna vingi sana havijafanya uchaguzi, lakini kwa hatua ya kwanza tunaanza na vyama 5 ambavyo hima hima wanatakiwa wafanye uchaguzi wao na ikifika tarehe 16-6- 2017 wawe wameshafikia pazuri kwenye uchaguzi”. Alisema Kweleza.
Vyama vitano (5) ambavyo vinaharakishwa kufanya uchaguzi ni Chama cha Basketball Zanzibar (BAZA), Chama cha Baskeli Zanzibar (CHABAZA), Chama cha Mpira wa Netball Zanzibar (CHANEZA), Chama cha Mpira wa Mikono Zanzibar yani Hand ball na Chama cha Mpira wa Meza Zanzibar yani Table Tennis.
Post a Comment