AZAM FC YAPATA MWALIKO MKOANI ARUSHA

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kufanya ziara maalumu ya siku tano mkoani Arusha ikitarajiwa kuelekea huko Mei 24 na kurejea Mei 29 jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo inatokana na mwaliko maalum waliopata kutoka Shule ya Trust St. Patrick, iliyopo maeneo ya Sakina mkoani humo, ambayo pia imesajiliwa kama kituo cha michezo.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema kuwa ziara hiyo itaambatana na mechi mbili za kirafiki zitakazotangazwa hapo baadaye pamoja na kuwapa pole wafiwa kufuatia ajali ya basi iliyotokea hivi karibuni iliyohusisha wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent.
“Tumealikwa na wenyeji wetu Arusha, watatugharamia kila kitu wao wametaka Azam FC iende kwa sababu muda mrefu hawajaiona na mashabiki wanahitaji kuiona, sisi tumeona tusiwanyime nafasi hii kwani wenzetu wapo kwenye kipindi kigumu sasa hivi hivyo wanahitaji kupata angalau burudani ndogo kuwaondoa kidogo katika majonzi waliyokuwa nayo,” alisema.
Huu ni mwendelezo mzuri wa Azam FC kuungana na jamii katika vipindi vya huzuni, itakumbukwa kuwa Novemba mwaka jana timu hiyo ilikwenda kuwapa pole waathirika wa tetemeko ardhi mjini Bukoba, mkoani Kagera, wakati ilipokwenda kupambana na Kagera Sugar na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

No comments