KOCHA WA AZAM AOMBA MUDA ZAIDI KUIJENGA VYEMA TIMU


KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kuwa anahitaji muda zaidi ili kukisuka kikosi chake na kucheza kupitia mifumo wanayoendelea kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo.
Zeben pia ametanabaisha kuwa atayafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon ulioisha kwa sare ya 1-1, ili waweze kufanya vizuri mchezo ujao dhidi ya Majimaji.
“Kwa sasa tunafanya tathimini ya mchezo uliopita, kutoa makosa na kurekebishana pale tulipokosea, tukimaliza hapo kwa wiki hii tutaanza kujipanga kwa mchezo ujao (Majimaji), lakini cha kwanza tunaangalia yali yaliyotokea katika mchezo wa kwanza, mapungufu yalikuwa wapi na nani anapaswa kufanya nini,” alisema
Azam FC kwa sasa ni miongoni mwa timu zilizoko nafasi ya nne hadi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, zote zikiwa zimekusanyia pointi moja kila mmoja zikizidiwa pointi mbili na vinara Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons, walijikusanyia pointi tatu.
Mechi vs Lyon
Akizungumzia mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon, Zeben alisema timu yake haikucheza vibaya sana kulingana na mechi zilizopita huku akidai kuwa tatizo kubwa linalokikabili kikosi chake ni ufungaji wa mabao.
“Hilo si tatizo sana kadiri muda utakavyokuwa ukienda, hali itabadilika, ni jambo la kuvuta subira na muda zaidi, ukipatikana muda wa kutosha basi timu itakuwa vizuri zaidi mpaka sehemu ya ushambuliaji,” alisema.
Mbali na hilo amesema kuwa wiki hii, atalifanyia kazi suala la wachezaji wake kushindwa kumaliza mechi kipindi cha kwanza, akidai kuwa kwa mechi kadhaa zilizopita kikosi chake kimekuwa kikitafuta ushindi kipindi cha pili kuliko mwanzoni mwa mechi.  
“Sikuwa na timu mwanzo, nimeingia kikosini hivi sasa na nimeanza kubadilisha mfumo na mbinu kwa timu kucheza namna tunavyotaka sisi kulingana na mifumo, hilo ni tatizo ambalo lipo ni kubwa kwa sasa na tunaendelea kujitahidi kulifanyia kazi na hata wiki hii tutaendelea nalo ili kwa mechi zijazo liweze kuondoka,” alisema.
Azam FC inakamiwa
Zeben aliendelea kusema kuwa jambo linaloonekana hivi sasa ni timu zote zinazokuja Azam Complex kucheza na timu yake, hufanya jitihada kubwa kuliko uwezo wao ili kuonyesha nao wanaweza kucheza mpira.
“Hili si tatizo kubwa sana inabidi tuendelee kulizoea na nitaendelea kuiboresha timu, ili kwa yoyote atakayekuja Chamazi au nje ya Chamazi tuweze kumfunga,” alisema.
Ligi itakuwa ngumu
Kocha huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema ameshuhudia mechi za kwanza za ligi msimu huu na kudai kuwa haitakuwa ligi rahisi sana na ngumu kwake yeye kutokana na kikosi alichonacho.
“Cha muhimu ni wachezaji kuendelea kushika mifumo yangu ninayoendelea kuwafundisha, kwa uzoefu wetu tuliokuwa nao hapa tumegundua timu yoyote inayocheza na Azam hata timu iwe kibonde vipi, basi itajitahidi kuweza kuweka rekodi, hili si tatizo sana tutaendele kupambana nalo kwa kuwa hii ni kazi yetu,” alisema.
Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, kitaanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Majimaji kesho Jumanne asubuhi, mechi itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.

No comments