ISMAIL GAMBO ATAMBA KUIFANYIA MAKUBWA KLABU YA AZAM FC


BEKI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Ismail Gambo, amewaahidi mashabiki wa timu hiyo mambo makubwa zaidi msimu huu kuliko yale anayoyaonyesha uwanjani hivi sasa.
Gambo ni miongoni mwa wachezaji watatu kutoka kikosi cha vijana cha Azam FC ‘Azam Academy’ waliochaguliwa kuchezea kikosi cha wakubwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, wengine ni mshambuliaji Shaaban Idd na kiungo Masoud Abdallah.
Mbali na hao, pia kocha huyo kutoka nchini Hispania, anaendelea kuwaangalia baadhi ya wachezaji wengine vijana wanaofanya mazoezi na kikosi hicho, ambao ni viungo Omary Wayne, Rajab Odasi na Prosper Mushi.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Gambo alisema atajitahidi kuongeza juhudi zaidi ili afanikiwe ili kupata nafasi ya kucheza timu ya Taifa na hatimaye kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.
“Najisikia vizuri kuwemo kwenye kikosi cha timu kubwa, hili ni jambo ambalo kila mchezaji hulitafuta kwa sababu ndio atatimiza malengo yake, huwezi kutimiza malengo kama unatokea benchi au hupati nafasi kabisa ya kucheza, mashabiki wa Azam FC watarajie mambo mazuri zaidi kutoka kwangu na hata kama kuna wakati nitafanya vibaya wasinivunje moyo waendelee kunipa moyo,” alisema.
Changamoto
Beki huyo aliyerejea akitokea Mwadui FC alikocheza msimu uliopita kwa mkopo, alisema bado anachangamoto kubwa ya kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kila mtu kuitolea macho nafasi hiyo.
“Hapa kuna wachezaji wengi wenye historia zao, lakini ukiwa mchezaji chipukizi una nafasi yako kwa hiyo siangalii huyu kacheza muda mrefu au ana uwezo mkubwa, nitajiangalia mimi kwa nafasi yangu ninayocheza kwa maana nina haki ya kuanza na nitaendelea kujifunza kila siku,” alisema.
Aliongeza: “Jambo kubwa ni kujiamini, kama kocha alivyompa nafasi hakuangalia uwezo wa mtu bali kaangalia umuhimu wa yule mchezaji wa kuwemo katika kikosi chake cha kwanza, kwa hiyo kwangu ni changamoto na mimi mwenyewe nafurahia kuwepo kwenye kikosi cha kwanza.”
Beki huyo hivi sasa amehamishwa namba kutoka beki wa kati hadi beki wa kulia, licha ya kutokuwa na uzoefu amekuwa akifanya vizuri jambo ambalo limemfanya kocha kumuamini na kumuweka kwenye orodha yake ya wachezaji 18 katika kila mchezo.
Moja ya mechi kubwa za mashindano alizocheza msimu hu ni ile Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, akicheza kwa dakika zote 90, mchezo ulioisha kwa Azam FC kuibuka mabingwa kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
Mbali na huo, pia alicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kwenye mchezo wa funguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon ulioisha kwa sare ya bao 1-1.  

No comments