AZAM FC YAISHUSHIA KIPIGO FRIENDS RENGERS

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanikiwa kuibuka na ushindi wa kishindo mbele ya timu ya Friends Rangers  baada ya kuichakaza mabao 6-0 katika mchezo wa kirafiki  uliochezwa katika Uwanja wa Azam complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezo huo uliochezwa jana kunako mishale ya sa moja jioni ulikuwa ni maalum kwa jili ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji huku pia ukiwa wa maandalizi kuelekea mtanange ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Lipuli utakaofanyika ndani ya dimba hilo Jumapili hii Septemba 24 mwaka huu.
Azam FC ilitakata vilivyo katika kila kipindi, ambapo ilijipatia mabao mawili ya uongozi kipindi cha kwanza kupitia kwa Nahodha wake, Himid Mao ‘Ninja’, aliyefunga la kwanza dakika ya 18 akimalizia pasi safi ya Yahya Zayd.
Mao alitupia jingine dakika 10 baadaye kwa njia ya mkwaju wa penalty kufuatia mshambuliaji Mbaraka Yusuph, kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati akienda kumtungua kipa wa Friends Rangers.
Kipindi cha pili Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alikibadilisha kikosi chote kilichoanza isipokuwa beki David Mwantika, aliyebakishwa na kuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya kupumzika dakika ya 79 na kuingia kiungo Salmin Hoza.
Katika kipindi hicho, Azam FC ilijiongezea mabao mengine manne na kuhitimisha ushindi huo, ambapo mshambuliaji Wazir Junior alihusika kwenye mabao mawili akifunga dakika ya 65 na 65.
Winga anayekuja kwa kasi Idd Kipagwile, aliipatia Azam FC bao la tano dakika ya 86 baada ya kuipokea pasi safi ya juu iliyopigwa na Hoza kabla ya kumpiga chenga kipa na kufunga bao hilo.
Ushindi huo ulihitimishwa kwa bao maridadi la Joseph Mahundi dakika ya 89, aliyeipokea pasi safi ya Hoza na kupiga shuti la umbali lililotinga wavuni.
Kikosi cha Azam FC mara baada ya mchezo huo kitaendelea tena na mazoezi kesho jioni kuendelea na maandalizi ya kuivaa Lipuli ya Iringa Jumapili hii.

No comments