MAGURI APINGANA NA VIONGOZI WA YANGA NA AZAM FC

Mchezaji anaecheza soka la kulipwa katika timu ya Dhofar SC ya nchini Omani,Elius Maguri amesema kwamba mchezaji anapomaliza mkataba wake wa awali ana haki ya kudai maslahi ambayo yataona yanafaa kwa upande wake ili asaini mkataba mpya.

Magurii ameyasema hayo kufuatia utaratibu uliowekwa na baadhi ya vilabu vya hapa nyumbani hasa Yanga na Azam ambao kwa nyakati tofauti viongozi wao walizungumza sera ya kubana matumizi.

"Mimi nafikiri hayo yatakuwa maamuzi ya mchezaji,kwa sababu kama mchezaji anaona thamani yake imepanda na anawindwa na baadhi ya timu kwa nini ashindwe kutaja dau lake ambalo anaamini litamfaa"alisema Maguri.

Aidha Maguri kwa upande mwingine alisema kwamba nao viongozi wa timu za hapa nyumbani ikiwemo Simba na Yanga wanashindwa kutenda kazi zao kwa ufasaha hasa wanaposhindwa kumpa mkataba mpya mchezaji wanaemuhitaji kabla ya mkataba wake kuisha.

"Mchezaji upo nae ndani ya klabu sasa kwa nini usianze kuzungumza nae mapema hadi usubiri mkataba wake ukaribie kwisha ndio juhudi za kumuongeza mkataba zinafanywa"aliongeza Maguri.

Maguri kwa sasa yupo nchini Afrika ya Kusini akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya COSAFA,ambayo Tanzania inashiriki kama nchi Mwalikwa.

No comments