AISHI MANULA ABEBA TUZO KWA MARA YA TATU MFULULIZO

Kipa namba moja wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aishi Manula, usiku wa kuamkia leo amefanikiwa kutwaa Tuzo ya Kipa Bora wa msimu huu (2016/17).
Mbali na kipa huyo kutwaa hiyo tuzo, pia ameingia kwenye kikosi bora cha msimu sambamba na beki kisiki wa kati wa timu hiyo, Yakubu Mohammed, huku mshambuliaji Shaaban Idd, akibeba Tuzo ya Ismail Khalfan U-20.
Aishi katika kipengele hicho aliwabwaga makipa wenzake, Juma Kaseja (Kagera Sugar) na Owen Chaima (Mbeya City), walioshindanishwa naye ili kupatikana kipa mahiri wa msimu.
Tuzo hii ya Kipa Bora, Aishi, ameitwaa kwa mara ya tatu mfululizo, mbili akitwaa msimu uliopita zikiwa ni za Kipa Bora wa Ligi Kuu na Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup).
Aidha kipa huyo namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, alianguka kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu baada yay a beki wa Simba, Mohammed Hussein, kuitwaa huku pia akiwashinda wengine watatu, Simon Msuva, Haruna Niyonzima (Yanga) na Shiza Kichuya (Simba).
Shaaban aliyetwaa tuzo hiyo ya kumuenzi mchezaji wa timu ya vijana ya Mbao, Ismail Khalfan, aliyefariki dunia uwanjani wakati wa mashindano ya Ligi ya Vijana Desemba mwaka jana, amewashinda Mosses Kitambi (Simba) na mchezaji mwenzake wa Azam FC, Abdallah Masoud ‘Cabaye’.
Tuzo nyingine
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, naye amefanikiwa kubeba Tuzo ya Kocha Bora wa msimu, akiwazidi Joseph Omog (Simba) na Ettiene Ndayiragije (Mbao).
Kiungo wa Yanga, Niyonzima, aliwabwaga Yusuph Ndikumana (Mbao) na Method Mwanjale (Simba) na kubeba Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni, huku mwamuzi Elly Sasii (Dar es Salaam) akiibuka kidedea kwa kuwa Mwamuzi Bora wa msimu dhidi ya wenzake Shomari Lawi (Kigoma) na Hance Mabena (Tanga).
Bao la kusawazisha alilofunga winga wa Simba, Shiza Kichuya dhidi ya Yanga kwenye sare ya bao 1-1, likiwa ni la mpira wa kona ya moja kwa moja kama alivyofanya Hood Mayanja mwanzoni mwa ligi dhidi ya Azam FC, limefanikiwa kuibuka kuwa bao bora la msimu.
Tuzo ya Mchezaji Bora Anayechipukia imekwenda kwa mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuf, akiwazidi Shaaban Idd (Azam FC) na Mohammed Issa (Mtibwa Sugar).
Nyota wa zamani wa Taifa Stars, Kitwana Manara, amefanikiwa kutwaa Tuzo ya Heshima, tuzo ambayo inaanzishwa kwa mara ya kwanza.
Kikosi Bora cha Msimu
Kikosi bora cha wachezaji 11 msimu huu ni kipa Aishi Manula (Azam FC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Mohamed Hussein (Simba), Yakubu Mohammed (Azam FC), Method Mwanjale (Simba), Kenny Ally (Mbeya City).
Wengine wanaounda kikosi hicho ni, Simon Msuva, Haruna Niyonzima (Yanga), Abdulrahman Musa (Ruvu Shooting), Mbaraka Yusuf (Kagera Sugar), Shiza Kichuya (Simba).

No comments