MCHA ATAMBA KUREJESHA KIWANGO CHAKE
Winga wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati, Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’, amesema kuwa kiwango kizuri
alichoanza kuonyesha hivi sasa ni mwanzo tu, na kutamba kuwa mashabiki wa timu
hiyo wakae mkao wa kupokea mambo makubwa zaidi kutoka kwake msimu huu.
Mcha
aliyeteswa na majeruhi ya goti kwa misimu miwili iliyopita kabla ya kurejea
dimbani mwishoni mwa msimu uliopita, ameanza kuonyesha cheche zake msimu huu
hasa katika mechi nne zilizopita alizoanzishwa kikosi cha kwanza.
Ndani ya
mechi hizo nne, Mcha amefanikiwa kufunga jumla ya mabao mawili katika mechi
dhidi ya Mbeya City (2-1) na Ruvu Shooting (2-2) na kuchangia pasi tatu za
mwisho za mabao katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
zinazoendelea kutimua vumbi.
Mabao
aliyotengeneza ni kwenye mechi dhidi ya Mbeya City akimtengenezea kwa krosi bao
alilofunga Gonazo Bi Ya Thomas, bao jingine alimsetia Fransisco Zekumbawira
wakati Azam FC ilipofungwa mabao 2-1 na Ndanda kabla ya Jumapili iliyopita
kufunga bao moja na kupiga kona iliyomaliziwa vema kwa kichwa na kiungo Jean
Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ dhidi ya Ruvu Shooting.
Mcha alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kufanikisha kurejesha makali yake huku akidai kuwa bila yeye asingeweza kufika
hapa.
“Nimegurahishwa
sana na kiwango nilichoanza kuonyesha hivi sasa, unajua sikuweza kucheza mechi
nyingi msimu uliopita baada ya kusumbuliwa na majeraha ya goti ambayo
yalinitesa sana kwa misimu miwili, niluirejea mwishoni na kujaribu kuisaidia
timu yangu, namshukuru Mungu kwa sasa nimeanza kurejea vizuri kwenye fomu
yangu, nawaahidi mashabiki makubwa zaidi,” alisema.
Alisema
anaendelea kufanya mazoezi kwa nguvu ili kujiweka fiti zaidi pamoja na kupokea
vema mafunzo bora wanayopewa na makocha wapya kutoka Hispania chini ya Kocha
Mkuu Zeben Hernandez na wasaidizi wake.
“Makocha
wanafanya kazi kubwa sana, nashukuru tunazidi kuimarika kila kukicha, naamini
tutafanya makubwa msimu huu, cha muhimu ni mashabiki kuendelea kuwa pamoja nasi
kwa nyakati zote za raha na shida, kwani hii ni timu yao na ipo kwa ajili yao,”
alimalizia Mcha.
Itakumbukwa kuwa mbali na Mcha kurejea mwishoni mwa msimu
uliopita, alifanikiwa kucheza dakika 691 za mashindano mbalimbali (sawa na
mechi saba na dakika 61) ambapo alifunga jumla ya mabao manne na kuchangia pasi
mbili za mabao
Post a Comment