KOCHA AZAM AKILI KUANZA KUONA MATUNDA YA MAFUNZO YAKE



 Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amepongeza ari ya kupambana iliyonyeshwa na wachezaji wake katika mechi zote mbili za mkoani Mbeya, huku akidai kuwa sasa mafunzo yao yameanza kuzaa matunda ndani ya kikosi hicho.
Hiyo inatokana na kikosi cha Azam FC juzi kukamilisha mechi zake mbili za mkoani Mbeya kwa kuzoa pointi zote sita, hasa baada ya ushindi dhidi ya Mbeya City (2-1) na ule wa kihistoria walioifunga Tanzania Prisons bao 1-0.
Pointi hizo sita zimeifanya Azam FC kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 10, ikiiacha Mbeya City katika nafasi ya pili na pointi zake saba sawa na Yanga na Simba, ambazo zina mchezo mmoja mkononi kila mmoja.
“Nawashukuru wachezaji kwa sababu mafunzo ambayo wamepokea tokea kipindi tunakuja yanaonekana yanazaa matunda kwa sababu kupata pointi sita ugenini hasa Mbeya ilikuwa ni kama historia.
“Lakini kiukweli kwa sasa hivi imekuwa ni kama kazi rahisi kwa sababu vijana wamejituma sana, na tulichowafundisha ndicho walichoenda kukitekeleza,” alisema.
Aliongeza kuwa : “Kazi imekuwa kubwa sana kwa sababu mpira ambao sisi kama makocha tulitegemea uchezwe, sio ule ambao umechezwa ukilinganisha na hali ya uwanja, lakini pia aina ya mazingira ambayo tumeweza kukutana nayo, ambayo yote ni tofauti sana na yale ambayo tumeyazoea Chamazi.”
Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, pia alichukua fursa hiyo kuwaelezea wachezaji wapya wa kikosi hicho walioanza kuichezea Azam FC jijini hapa, beki Daniel Amoah na mshambuliaji Gonazo Bi Thomas, akisema kuwa ni wachezaji wazuri.
“Ni wachezaji ambao nao wameonyesha uwezo wao, mazoezi waliyokuwa wakiyapata ingawa kwa kipindi kifupi wamejaribu kuyafanyia kazi, ingawaje kwa wao kazi imekuwa ni ngumu kidogo na hii ni kwa sababu bado hawajaweza kuzoeana na wenzao,” alisema.
Azam FC inataraji kushuka tena dimbani Septemba 17 mwaka huu kuvaana na Simba katika mchezo unaotaraji kua na ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora uliopo kwa timu hizo.

No comments