KOCHA AZAM FC AHITAJIN MECHI 4 ZA KIRAFIKI
Cioaba ameweka wazi kuwa kikosi chake kitaendelea na mazoezi mara mbili kwa siku na kucheza mechi nne kali za kirafiki hadi michuano hiyo itakapomalizika wiki mbili zijazo kabla ya ligi kuendelea.
“Umeona baada ya mechi ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar niliwapa mapumziko baadhi ya wachezaji kwa siku nne kwa ajili ya kupumzika, kwa sababu nina wiki tatu za maandalizi kuelekea mchezo ujao kwa sasa nasubiria programu kutoka TFF.
“Tunaendelea na mipango yetu, kila siku tutakuwa na mazoezi mara mbili asubuhi na jioni na kwenye wiki tatu hizi nitaweka mechi nne za kirafiki hapa Chamazi dhidi ya timu nzuri ili kumuona mchezaji mpya aliyekuja (Bernard Arthur) na kwa ajili ya maandalizi ya hapo baadaye,” alisema Cioaba.
Cioaba alisema mchezo wa kwanza wa kirafiki utafanyika Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex na kudai kwa uongozi unatafuta timu ya kucheza nao.
“Nahitaji timu nzuri na imara ya kucheza nayo hapa kwa mechi zote hizo nne, mechi nyingine itakuwa baada ya siku tatu, kila baada ya siku tatu nitakuwa na mechi ya kirafiki hapa Chamazi amekuja mshambuliaji mpya Bernard nataka aingie kwenye timu na kufanya muunganiko na baadhi ya wachezaji na wamjue kwa haraka, ana ubora gani kwenye mechi,” alisema.
Asifu kutokuwa na majeruhi
Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana alishukuru kuona kikosi chake mpaka sasa kimecheza jumla ya mechi 11 za kwanza za ligi bila kuwa na majeruhi.
“Hili ni jambo zuri kwa kuwa hapo baadaye tutakuwa na timu yote,” alisema.
Kutetea Mapinduzi Cup
Baadaye mwaka mwezi huu, Azam FC inatarajia kuelekea visiwani Zanzibar kwenda kupigania taji la Mapinduzi Cup ililolitwaa mwaka huu, akizungumzia ujio wa michuano hiyo Cioaba amedai anakwenda kutetea kombe hilo.
“Unaona baada ya wiki tatu hizi ligi kusimama, tutakuwa na programu ngumu tutatakiwa kucheza mechi za ligi na baadaye tutakwenda Zanzibar kwenye kombe (Mapinduzi Cup) kucheza mechi, nataka kwenda kama tulivyochukua kombe msimu uliopita basi tuchukue tena.
“Lakini nitapenda kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji ambao hawajacheza kwenye ligi wacheze kwenye kombe hilo ili kuona ubora wao,” alisema.
Radhi kwa mashabiki
Cioaba aliwaomba radhi mashabiki wa Azam FC kutokana na sare ya bao 1-1 waliyopata kwenye mchezo wa uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar, akisema kuwa licha ya matokeo hayo bado wapo nafasi sawa na Simba inayoongoza wote wakijikusanyia jumla ya pointi 23.
“Hii ni nzuri kwa kuwa mnafahamu kuwa hii ni timu mpya na inapigana kwa hiyo nafasi, namuahidi kila mmoja kama nikiendelea kuwa hapa kwenye hii timu sitakuwa chini kwa kuwa timu inapenda kupambana kwenye kila mechi kwa ajili ya kukaa kwenye nafasi hiyo, daima timu yangu haitakuwa chini hapo baadaye,” alisema.
Azam FC imejikusanyia pointi hizo katika nafasi ya pili baada ya kushinda mechi sita na kutoka sare mara tano huku ikiwa ndio timu pekee iliyoruhusu mabao machache ikiwa imecheza michezo 11 na kufungwa mabao matatu pekee.
Post a Comment