KAMATI YA SAA 72 YATOA MAAMUZI MAZITO KWA TIMU YA PRISONS
KAMATI ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Novemba 22, 2017 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi kwa msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.
Klabu ya Tanzania Prisons imepewa Onyo Kali kwa kuwakilishwa kwenye benchi na ofisa tofauti na yule aliyeudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) cha mchezo kati yake na Kagera Sugar uliofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Katika kikao hicho, Prisons iliwakilishwa na Meneja wake Erasto J. Ntabah lakini kwenye benchi alikaa Hassan Mtege. Adhabu ya Onyo Kali kwa klabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Pia Erasto J. Ntabah amesimamishwa hadi suala lake la kutoka jukwaani na kwenda kumfokea Mwamuzi wa Akiba litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Amesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Mchezaji Benjamin Asukile wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu na Mwamuzi kwa kosa la kumpiga kiwiko kwenye paji la uso mchezaji wa Kagera Sugar.
Kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuwafuata waamuzi na kuwalalamikia kwa kurusha mikono akionyesha kutoridhika na maamuzi yao. Alifanya hivyo kwenye mechi namba 69 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Ruvu Shooting iliyofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex na adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, Klabu ya Mvuvumwa imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa timu yake kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya African Lyon ikiwa na maofisa pungufu, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza. Mechi hiyo ilifanyika Novemba 7, 2017 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mtunza Vifaa wa timu ya JKT Mlale, Noel Murish amesimamishwa hadi suala lake la kuwamwagia maji washabiki wa Polisi Tanzania litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha ni kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi. Alifanya kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Klabu ya Coastal Union imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi ikiwa na maofisa pungufu, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza. Ilifanya hivyo katika mechi dhidi ya JKT Mlale iliyofanyika Novemba 12, 2017 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo Klabu ya JKT Mlale imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza.
JKT Mlale imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya KMC kumchezesha nahodha wake Stephano Mwasika katika mechi namba 28 iliyofanyika Oktoba 30, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati akiwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Mwasika alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko mpinzani wake kwenye mechi namba 15 kati ya KMC na Mbeya kwanza iliyochezwa Oktoba 5, 2017 katika Uwanja wa Azam Complex.
Baada ya kupata kadi hiyo, Mwasika alitakiwa kukosa mechi tatu na kulipa faini ya sh. 300,000 (laki tatu). Mechi alizotakiwa kukosa ni dhidi ya Mufindi United (Oktoba 15), Polisi Tanzania (Oktoba 23) na JKT Mlale (Oktoba 30). Alikosa mechi mbili tu za kwanza, lakini akacheza mechi ya tatu dhidi ya JKT Mlale iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Klabu ya Toto Africans imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa kikao cha maandalizi (pre match meeting) katika mechi dhidi ya Biashara United Mara iliyofanyika Novemba 5, 2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. Adhabu hiyo ni utekelezaji wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Meneja wa Toto Africans, Yusufu Jumaa amefungiwa miezi miwili na kupigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya kuondolewa na Mwamuzi kwenye benchi la ufundi kwa kupinga maamuzi yake na kumshambulia kwa maneno.
Ofisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet amesimamishwa hadi suala lake la kummwagia maji Mwamuzi na kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali wakati wa mapumziko katika mechi hiyo litakaposilikizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Waamuzi Wasaidizi Jumanne Njige wa Mwanza na Bam Bilasho wa Dodoma wamepewa Onyo Kali kwa kuchezesha chini ya kiwango mechi namba 36 ya Kundi C kati ya Transit Camp na Rhino Rangers iliyofanyika Novemba 11, 2017 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Post a Comment