WANAWAKE 28 WAHITIMU KOZI YA UKOCHA TFF

Makocha 28 wanawake kutoka vyuo mbalimbali vya Maendeleo ya Jamii nchini leo Oktoba 17, 2017 wamehitimu kozi fupi ya ukocha katika kozi iliyoratibiwa kwa pamoja kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO).

Kozi hiyo ya siku mbili ambayo ni ya pili kufanyika kwa makocha hao, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume - Makao Makuu ya TFF ilikuwa chini ya mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.

Akizungumza kwenye ufungaji wa kozi hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo amesema Serikali inafahamu kuwa inatakiwa kuwekeza kwenye soka la wanawake kuanzia upande wa vijana na ndio maana inatengeneza mazingira na sera zitakazowezesha mafanikio hayo.

Singo amesema nchi mbalimbali wana maendeleo makubwa katika mpira wa miguu kwa wanawake na sasa wakati wa Tanzania kuwekeza katika upande huo kuanzia kwa watoto na makocha.

Kadhalika, Singo amewataka wahitimu kuchukuwa mafunzo hayo kwa uzito mkubwa kwa sababu mpira wa miguu ya ajira na elimu hiyo itaongeza kitu kikubwa kwao.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Mpira wa la Wanawake (TWFA), Amina Karuma amesema lengo la chama chake na TFF kuhakikisha soka linachezwa nchi nzima linaelekea kutimia.

Amewataka wahitimu hao wa kozi hiyo fupi kuvitumia vyeti walivyovipata kuendeleza soka la wanawake na kufanyia kazi yale yote waliyofundishwa.

Pia ameiomba Serikali kuwaunga mkono katika maendeleo ya soka la wanawake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ufundi wa TFF Salum Madadi amesema kufundisha watoto kuna changamoto nyingi, lakini makocha hao wamefundishwa maarifa ya jinsi ya kukabiliana nazo.

Amesema maarifa hayo sio makocha wote wanaweza kuyapata lakini wameona umuhimu mkubwa kwa wahitimu hao kuweza kuyapata ili kwenda kuibua vipaji kuanzia chini.

Wahitimu wa kozi hiyo wamepatiwa vyeti vya ushiriki na vifaa vya michezo ikiwemo koni na mipira.

No comments