KESI INAYOWAKABILI VIONGOZI WA JUU WA SIMBA YAPIGWA KALENDA

Na Unique Maringo
WAKILI wa Serikali Estazia Wilson ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi katika kesi
ya kutakatisha fedha na kugushi inayomkabili Rais wa  Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange `Kaburu` kuwa upelelezi unaendelea na kwamba kuna nyaraka mbalimbali zimepelekwa kwa mtaalamu wa maandishi.

Alidai kuwa shauri hilo limekuja kwaajili ya kutanjwa ambapo wanasubiri ripoti ya polisi.
Wakili upande wa utetezi Evidius Mtawala aliomba tarehe ya karibu ili upande wa mashtaka uweze kukamilisha upelelezi huo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa aliutaka upande wa jamuhuri kujitahidi kuharakisha upelelezi kwasababu washtakiwa wapo ndani na kwamba wajitahidi kufuatilia ripoti hiyo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 8 mwaka huu kwaajili ya kutanjwa.

Evans Elieza  Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha USD 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata USD 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha,Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidiaAveva  kujipatia USD 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

No comments