GOR MAHIA NA AFC LEOPARDS KUMENYANA JUMAPILI

Mchezo wa ligi kuu nchini Kenya kati ya watani wa jadi Gor Mahia na AFC Leopards, utachezwa siku ya Jumapili licha ya hapo awali kuahirishwa kwa sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na RFI Kampuni ya KPL inayosimamia ligi kuu ya soka nchini humo imeeleza kuwa AFC Leopards imefanikiwa kuupata uwanja wa taifa wa Nyayo kuandaa mchuano huo maarufu kama Nairobi Derby au Mashemaji Derby.
Mchuano huu awali ulikuwa umepangwa kufanyika katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru, lakini uongozi wa soka ukaamua kuahirisha kwa sababu za kiusalama kutokana na wingi wa mashabiki wa timu hizo mbili.
Kanuni za ligi kuu ya soka nchini humo, zinaitaka klabu mweyeji kuhakikisha kuwa inashughulikia maswala ya usalama na mambo mengine.
Viwanja viwili vikubwa nchini humo Kasarani na Nyayo vilivyo jijini Nairobi, vimefungwa kwa maandalizi ya michuano ya mataifa bingwa barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN.
AFC na Gor Mahia vitamenyana kwa mara ya 83 katika historia ya ligi kuu ya soka nchini humo.
Uongozi wa klabu ya AFC umetoa wito kwa mashabiki wake kujitokeza kwa wingi, kuishabiki klabu yao maarufu kama Ingwe.
Gor Mahia ambao ni mabingwa wa mwaka 2015, ni wa pili latika msururu wa ligi hiyo kwa alama 16 baada ya mechi nane, huku AFC Leopards ikiwa ya nne kwa alama 14 baada ya mechi nane pia.

No comments