KENYA YANG'ARA KWA JUDO, ZANZIBAR YASHIKA NAFASI YA 3 WENZAO BARA WA MWISHO

Na: Sleiman ussi haji, Zanzibar.
Mashindano ya 11 ya Judo ya Afrika Mashariki na Kati yamemalizika siku ya jana jioni  katika Ukumbi wa Judo uliopo Aman Mjini Unguja ambapo Kenya wameongoza huku Burundi wakishika nafasi ya pili na wenyeji Zanzibar wamekamata nafasi ya tatu huku timu ya Tanzania bara ikishika nafasi ya mwisho katika ushiriki wa mashindano hayo.

Kenya imeongoza ikishinda Medali za dhahabu (Gold) 4, Fedha (Silver)1 na Shaba (Bronze) 8 huku Burundi ikishika nafasi ya pili baada ya kushinda Medali za Dhahabu 3, Fedha 3 na Shaba 2 huku wenyeji wa Mashindano hayo Zanzibar ikishika nafasi ya tatu baada ya kupata Medali ya Dhahabu 1, Fedha 2 na Shaba 2 na timu ya mwisho katika Mashindano hayo ni Tanzania Bara waliyoambulia Medali moja ya Fedha na moja ya Shaba.

Wachezaji wa Kenya walioshinda Medali za Dhahabu katika Mashindano hayo ni George Kimani kwa wanaume wenye uzito wa kilo 100, Johnstone Kirimi kilo 90, na kwa Wanawake ni Esther Ikiugu uzito wa kilo 63 na Alice Chebet Muragu kilo 78.

Burundi ambao wamekamata nafasi ya pili wachezaji wao walioshinda Medali za Dhahabu kwa Wanaume ni Samuel Kwitonda uzito wa kilo 81 na kwa upande wa Wanawake ni Angeciella Niragira uzito wa kilo 70 pamoja na Enia Irakole kilo 78 wakati Zanzibar alipata Medali ya Dhahabu ni Masoud Amour Kombo pekee aliyeshinda kwenye uzito wa kilo 100 ikiwa ni mara yake ya 10 mfululizo katika mashindano hayo.

Kumalizika kwa mashindano hayo ya 11 ni matayarisho ya Mashindano ya 12 ya Afrika Mashariki na kati ambapo kwa msimu ujao yatafanyika Nairobi Nchini Kenya mwakani.

No comments