MALIMA AMPONGEZA MWIGULU NCHEMBA
Mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya Yanga,Bakali Malima amempongeza waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba kwa kufanya kazi kubwa ya kumrejesha kocha Hans van der Pluijm kuendelea kuifundisha timu hiyo.
Malima amesema kwamba Mwigulu amefanya kazi kubwa na anapaswa kupongezwa kwani hatua ambayo ameifanya ni nzuri kwa kuwa viongozi wa Yanga walifanya makosa kuachana na kocha huyo ilihali amekuwa na mafanikio makubwa ndani ya timu.
Amesema kwamba kwa sasa uongozi wa Yanga hauna watu wanaojua mpira hasa kaimu katibu mkuu wa klabu Baraka Deusdedit kwani kwa kutumia nafasi yake ameshindwa kuona nini umuhimu wa kocha huyo aliyeipeleka timu kwenye hatua ya makundi katika kombe la shirikisho barani Afrika.
Katika hatua nyingine Malima amesema kwamba ingawa kocha Hans amerejea ndani ya klabu hiyo lakini pia nae anatakiwa kubadilika katika mfumo wa ufundishaji wake kwani kuna mapungufu kazaa ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho.
Amedai kuwa Hans anatakiwa apate mshauri mwenye uelewa mkubwa wa maswala ya mpira kama ilivyo awali wakati alipokuwa na kocha wa timu ya Taifa Chars Boniphace Mkwasa.
Hata hivyo amedai kuwa kwa sasa kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mwambusi anatakiwa kwenda kupata ushauri kwa Mkwasa ili ampe mawazo ambayo yeye yalimsaidia wakati alipokuwa chini ya kocha huyo.
Post a Comment