LIGI YA TAIFA WANAWAKE KUANZA RASMI KESHO

Ligi ya Taifa ya Wanawake inatarajiwa kuanza kesho Jumanne Novemba 1, 2016 kwa viwanja sita kuchezwa mechi za ufunguzi ingawa hafla ya uzinduzi wa ligi hiyo utafanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma katika mchezo ambao Baobao ya hapo itakapocheza na Victoria Queens ya Kagera.
Ligi hiyo ya kwanza kufanyika nchini Tanzania, lakini pia kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati imetokea kuvutia wadau kadhaa wakiwamo Azam Tv ambao wamedhamini kwa kuonyesha mubashara (live), michezo hiyo 30 itakayofanyika viwanja mbalimbali hapa nchini.

Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo mawaziri na wabunge ambao kwa sasa wako kwenye vikao mjini Dodoma kwa pamoja wanatarajiwa kuwa katika hafla hiyo ambayo pilikapilika zake zinatarajiwa kuanza saa 8.00 mchana kabla ya mchezo kuanza saa 10.00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
TFF imepeleka uzinduzi huo Dodoma ikiwa na lengo la kuhamasisha soka mikoani tofauti na Dar es Salaam ambako ilizoeleka zaidi miaka ya nyuma kabla ya kuwa na mpango wa mashindano ya aina hiyo yanayoshirikisha timu 12 kutoka kona mbalimbali za nchi.
Kadhalika, kwa siku ya Novemba mosi ya uzinduzi huo vingozi wengi wa Serikali wakiwamo wabunge wanatajiwa kuwa Dodoma ambako watapata fursa pekee ya kushuhudia burudani ya mpira wa miguu wa ushindani itakayosukuma hamasa ya kutoa michango yao mbalimbali kwa ajili ya soka la wanawake.
Mbali ya mchezo huo wa kundi B kati ya Baobao na Victoria, michezo mingine itakuwa ni kati ya Sisterz na Panama utakaofanyika Uwanja wa Tanganyika huko Kigoma wakati Marsh Academy ya Mwanza itacheza na Majengo Women ya Singida kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kundi A kutakuwa na michezo mitatu ambako Viva Queens ya Mtwara itacheza na Mburahati Queens ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati Fair Play ya Tanga itapambana na Evergreen ya Dar Salaam katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga huku JKT Queens ikiwa ni wenyeji wa Mlandizi Queens ya Pwani kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam

No comments