KAPOMBE MBIONI KUCHEZA MECHI DHIDI YA YANGA


BEKI wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, ameweka wazi kuwa afya yake inaendelea vizuri baada ya kufanikiwa kurejea dimbani huku akidai kuwa Mungu atamsaidia kuweza kucheza mechi dhidi ya Yanga.
Mchezo huo ni ule wa Ngao ya Jamii wa kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumatano Ijayo Agosti 17 mwaka huu.
Beki huyo kisiki mwenye kasi ya aina yake na uwezo wa kufunga mabao, amerejea dimbani katikati ya mwezi uliopita baada ya kupona ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu) uliomweka nje ya dimba kwa takribani siku 122 tokea Aprili 2 mwaka huu.
Mpaka sasa wakati Azam FC ikiwa kwenye maandalizi ya msimu mpya, beki huyo amefanikiwa kucheza mechi mbili za majaribio kwa takribani dakika 65, ya kwanza dhidi ya JKT Ruvu aliingia dakika 20 za mwisho za kipindi cha pili kabla ya kukipiga kwa dakika 45 walipocheza na Ruvu Shooting Jumamosi iliyopita.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kapombe alisema atendelea kujiweka fiti mazoezini na anaamini ataweza kuiongoza timu hiyo katika mchezo huo unaotarajia kuwa upinzani mkubwa kwa pande zote mbili.
“Kwa mimi namshukuru Mungu kuweza kucheza mechi mbili zilizopita japo si kwa dakika 90, Mwenyenzi Mungu amenijaalia niweze kufikia hapa nilipo, pia siwezi kumsahau mke wangu, kwani ndio amekuwa mchango mkubwa kwangu kwani toka naumwa hadi napona hivi sasa alikuwa pamoja nami na kunipa ushauri mwingi.
“Kwa sasa naendelea kufanya mazoezi, kocha anaendelea kunipa mazoezi na mengine yakiwa ni ya ziada ili niweze kurejea kwenye hali yangu ya kawaida, lakini naendelea kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipigania mpaka hapa nilipo pamoja na watu wengine wote ambao wameweza kufanya mchango wao mpaka nafika na kuanza kucheza tena,” alimalizia Kapombe.
Beki huyo wa zamani wa Simba na AS Cannes ya Ufaransa, amekuwa na kiwango kizuri msimu uliopita, kwani mbali na kulinda vema safu ya ulinzi ya Azam FC pia aliweza kuweka jitihada na kufunga mabao 11 kwenye mashindano yote waliyoshiriki, akitupia nane (Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara), mawili Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na moja ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC) wakati timu hiyo ikiilaza Bidvest Wits mabao 3-0.

No comments