AZAM FC KUCHEZA NA URA SIKU YA IJUMAA
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kucheza mchezo wa kwanza wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam keshokutwa Ijumaa.
Hiyo itakuwa ni mechi ya nane ya kirafiki kwa Azam FC katika kujiandaa vema na msimu ujao, imefanikiwa kushinda mechi tano na sare mbili dhidi ya JKT Ruvu (1-1) na Ruvu Shooting (1-1).
Huo ndio utakuwa mchezo wa mwisho wa kirafiki kwa Azam FC kabla ya kuanza mikikimikiki ya msimu ujao, wakianza kucheza dhidi ya Yanga Agosti 17 mwaka huu katika mechi ya Ngao ya Jamii inayofungua msimu mpya.
Akizungumzia mchezo huo leo mara baada ya mazoezi ya asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC Zeben Hernandez, alisema haichukulii uzito mkubwa mechi hiyo bali anachoangalia kwa sasa ni kushinda dhidi ya Yanga.
“Naandaa timu kwa sasa ili niweze kupambana nao na kuweza kupata kiwango cha kuja kucheza na Yanga, baada ya kucheza na Yanga tutaendelea na mfumo ule ule tulioanza nao wa kuboresha timu ili iweze kuwa bora zaidi hapo baadaye,” alisema.
URA ambayo nayo ipo kwenye maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu Uganda, ni kipimo kizuri kwa Azam FC kutokana na timu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya tano msimu uliopita ikijikusanyia pointi 47, pointi 10 nyuma ya mabingwa KCCA.
Post a Comment