YONDANI ASIMAMISHWA KUCHEZA SOKA BAADA YA KUMTEMEA MATE ASANTE KWASI
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa) katika kikao chake cha Mei 1, 2018 chini ya Mwenyekiti wake Bw. Clement Sanga ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, na malalamiko ya klabu za Yanga na Arusha FC na kuyafanyia uamuzi.
Mechi namba 199 (Mbeya City 1 vs Yanga 1). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na vurugu za washabiki wake ikiwemo kurusha mawe na chupa uwanjani katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 22, 2018 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Kwa vile mchezaji Obrey Chirwa wa Yanga alionywa kwa kadi ya njano kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Mbeya City ingawa kwenye picha za televisheni inaonekana kama alipiga kiwiko, Kamati haikutoa adhabu nyingine kwa vile tayari ameadhibiwa.
Hata hivyo, klabu ya Yanga imeandikiwa barua kuhusu kumuonya mchezaji huyo kwa vile kumbukumbu zinaonyesha ameshafanya matukio ya utovu wa nidhamu mara kadhaa akiwa uwanjani.
Mechi namba 178 (Simba 1 vs Yanga 0). Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amesimamishwa hadi suala lake la kumtemea mate Asante Kwasi wa Simba katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 29, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Adhabu ya kusimamishwa imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.
Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepewa Onyo Kali kwa kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yake baada ya mchezo kumalizika. Kitendo chake ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Post a Comment