RASMI AZAM FC WATANGAZA KUMALIZANA NA DONALD NGOMA
Baada ya kuingia makubaliano hayo, muda wowote kuanzia sasa Azam FC inatarajia kumpeleka mchezaji huyo katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya afya ili kuona ni kwa kiasi gani majeraha yaliyokuwa yakimsumbua yamepona.
Kwa mujibu wa taarifa hii ambayo imeandikwa katika wavuti ya klabu hiyo,Azam FC inaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo kutoka nchini Zimbabwe aliyewahi kuchezea FC Platinum ya huko kabla ya kuhamia Yanga, ni sehemu tu ya mikakati ya benchi la ufundi na uongozi katika kuboresha kikosi kwenye eneo la ushambuliaji kuelekea msimu ujao.
Aidha kama mambo yataenda vizuri, uongozi wa Azam FC unaamini kuwa Ngoma atakuwa ni miongoni mwa nyota wapya wa timu hiyo watakaoonekana kwenye Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup) linalotarajia kuanza hivi karibuni wakiwa kama mabingwa watetezi wa michuano hiyo.
Tayari mchezaji huyo ameandaliwa jezi namba 11 iliyokuwa ikitumiwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, aliyerejea Aduana Stars ya nchini kwao Ghana.
Klabu hiyo inawaomba mashabiki wa Azam FC wawe watulivu katika kipindi hiki na kuendelea kuisapoti timu, kwani uongozi umejipanga kufanyia kazi ripoti ya benchi ya ufundi na kuboresha kikosi ili kusaka taji la ubingwa msimu ujao.
Post a Comment