MAJERAHA YAMENIHARIBIA;SHABANI IDD
MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Shaaban Idd, amekiri kuwa kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi saba akiuguza majeraha ya nyonga kulimwaribia kuendeleza kasi aliyokuwa nayo msimu uliopita.
Usiku wa kuamkia leo, Shaaban ameiongoza Azam FC kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) akifunga hat-trick na jingine likitupiwa wavuni na kiungo Frank Domayo.
Mara baada ya Shaaban kukosa raundi ya kwanza ya ligi kutokana na majeraha aliyopata mwishoni mwa msimu uliopita, hivi sasa amerejea vema kabisa baada ya hat-trick hiyo kumfanya akikishe mabao nane kwenye ligi msimu huu, huku akiandika rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya mechi nne zilizopita.
Mabao hayo nane yamemfanya kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita alipopandishwa timu kubwa akitokea Azam B, na kufunga mabao sita kwenye msimu wake wa kwanza wa ligi.
Shaaban alisema ilimlazimu kuvuta subira ili kurejea kwenye ubora wake na anamshukuru Mwenyezi Mungu hivi sasa ameanza kufanya vizuri huku akiahidi makubwa zaidi msimu ujao.
“Mimi sikuanza msimu kwenye raundi ya kwanza ila nimerudi raundi ya pili, nimekaa nje ya dimba zaidi ya miezi sita kwa hiyo nipate ile kasi yangu ambayo nilimaliza nayo msimu ulioisha ilibidi ichukue muda na lazima iwe hivyo kwa sababu mpira ni mchezo unaohitaji utulivu wa akili, utimamu wa mwili.
“Miezi sita si midogo kwa sababu sikuruhusiwa hata kugusa mpira, haikuwa na maana kwamba kiwango changu kimeshuka bali nilikuwa kwenye njia ya kunifanya mimi nifanye kazi kwa bidii ili kurejea katika kiwango ambacho nilikuwa nacho, namshukuru Mungu nimejitahidi na ndio kama unavyoona nimechanganya kwenye mechi za mwisho,” alisema.
SOURCE Mtandao wa klabu ya Azam FC.
Post a Comment