UNAI EMERY NDIE MRITHI WA ARSENE WENGER

Unai Emery ametangazwa kuwa meneja mpya wa Arsenal na afisa mkuu mtendaji wa klabu hiyo Ivan Gazidis.

Bw Gazidis amesema Emery amepewa fursa ya kipekee ya kuongoza "sura mpya" yaklabu hiyo ya England.

Emery, 46, amejiunga na Gunners baada ya kuondoka PSG ambapo aliwaongoza kushinda ligi kuu ya Ufaransa, Ligue 1.
Mhispania huyo pia alishinda vikombe vya ligi mara nne akiwa na miamba hao wa Ufaransa.

Awali alikuwa meneja wa Sevilla ambapo aliwasaidia kushinda Europa League mara tatu mtawalia.

Atamrithi Arsene Wenger ambaye aliondoka klabu hiyo baada ya kuwaongoza kwa miaka 22.
"Unai ana historia nzuri nzuri ya ufanisi katika maisha yake kama mkufunzi, amewakuza wachezaji wengi sana wenye vipaji Ulaya na kucheza mchezo wa kuvutia ambao unaingiana vyema na Arsenal," Gazidis ameongeza.

"Bidii yake na mtazamo wake wa kufurahia zaidi kazi yake pamoja na maadili ndani na nje ya uwanja vinamfanya kuwa mtu bora zaidi wa kutupeleka mbele."
Meneja wa msaidizi wa Manchester City ambaye pia ni nahodha wa zamani wa Arsenal Mikel Arteta alipiga upatu sana kumrithi Wenger.
Lakini Emery, ambaye hana ufahamu sana wa Kiingereza, ndiye aliyeteuliwa.

Ataongoza Arsenal hadi kwenye enzi mpya baada ya kuondoka kwa Wenger, 68, aliyeshinda mataji matatu ya Ligi ya Premia na vikombe saba vya FA akiwa na klabu hiyo.

"Nina furaha sana kukabidhiwa wajibu huu wa kuanza ukurasa huu mpya katika historia ya Arsenal," amesema Emery.

"Nina furaha sana kujiunga na moja ya klabu bora zaidi katika mchezo huu. Arsenal wanafahamika na kupendwa kote duniani kwa mtindo wao wa uchezaji, kujitolea kwao kukuza wachezaji chipukizi, uwanja wao mzuri na jinsi klabu hii huongozwa.

"Nafurahia sana kwa yale tunaweza kutimiza pamoja na nasubiri kwa hamu kuwapa wanaoipenda Arsenal kumbukumbu nzuri."

SOURCE BBC.

No comments