KARIA AELEZA SABABU ZA KUMTEUA WILFRED KIDAO

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini TFF Wallace Karia amesema kwamba aliamua kumpa nafasi Wilfred Kidao kukaimu nafasi ya katibu mkuu wa TFF kwa kua alibaini kiongozi huyo analijua vizuri shirikisho hilo pia kuwa na sifa zote za kuwa kiongozi katika sehemu hiyo.

Akiongea mbele ya Wahariri wa vyombo vya Habari leo hii Karia alisema kwamba wajumbe wa kamati ya utendaji chombo ambacho kina husika na kupitisha kilibariki awe kaimu katibu mkuu wa TFF.

"Kutoka nje ya Ofisi na kukaimu hii siyo mara ya kwanza,wakati ndugu Tenga anashinda Uraisi alimuomba Bi.Lina Kessy ambaye alikuwa mtumishi wa Serikali kuwa maratibu wa Ofisi,nafasi iliyokuwa kama mkuu wa sekretarieti wakati huo"alisema Karia.

Alisema kwamba Katiba ya TFF inahitaji Rais wa TFF atoe mapendekezo ya Katibu mkuu ili kamati ya utendaji ijadili, na maswala hayo yanafanyika kwa sababu Rais kama msimamizi wa Sektretarieti anafanya kazi kwa karibu sana na katibu mkuu hivyo FIFA wanahitaji watu hao wanaoweza kufanya kazi kwa karibu,ndipo Rais wa TFF anapopewa kipaumbele cha mtu wa kufanya naye kazi.

Hata hivyo Karia alisema kwamba kikao kijacho cha kamati ya utendaji kitaamua njia sahihi ya kupata katibu mkuu na watanzania watarajie kuwa katibu mkuu atapatikana ndani ya muda mfupi baada ya kikao cha kamati ya utendaji.

No comments