JKU WASEMA WAKO TAYARI KUWAVAA ZESCO UNITED

Na Sleiman Ussi,Zanzibar
Katibu mkuu wa timu ya JKU ya Zanzibar,Saad Ujudi amesema kwamba kikosi chake kimejipanga vyema kuwakabili Zesco United ya nchini Zambia katika mchezo wao wa kombe la klabu bingwa barani Afrika utakaopigwa siku ya jumamosi kwenye uwanja wa Amani.

Ujudi alisema kwamba wanaiheshimu timu ya Zesco United kutokana na uzoefu wao katika michuano ya kimataifa lakini hicho sio kikwazo chao wao kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye pambano hilo.

Alisema kwamba wachezaji wote wapo kambini na wanahudumiwa kwa ustadi mkubwa kuelekea kwenye pambano hilo na jambo la faraja ni kuona kila mchezaji ana hamasa ya kucheza pambano hilo la kimataifa.

Tayari Zesco United imeshawasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya pambano hilo ambalo linataraji kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili.

No comments