WACHEZAJI AZAM FC WAWAPA FARAJA MASHABIKI KABLA YA MECHI YA SIMBA

ZIKIWA zimesalia siku mbili kabla ya Azam FC kupambana na Simba, nahodha msaidizi wa timu hiyo Agrey Moris, ameweka wazi kuwa hawatawaangusha mashabiki kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumatano saa 10.00 jioni, unatarajia kuwa mkali ya wa aina yake kutokana na Azam FC iliyojikusanyia pointi 33 kuwa kwenye vita kali ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo dhidi ya wekundu hao walio kileleni kwa pointi 38.
 Moris aliwataka mashabiki kuondoa hofu na kuwaomba kujitokeza kwa wingi uwanjani kwenye mchezo huo ili kuwapa sapoti.
“Kwanza tunamshukuru Mungu wachezaji wako katika morali ya hali ya juu yaani inaonyesha wachezaji kila mmoja anajiandaa kuhakikisha kutaka kushinda mchezo huu,” alisema.
Moris alikiri ushindani utakuwa mkubwa kutokana na Simba kuwa kileleni mwa ligi, na kudai kwa sasa timu yake imeongezewa morali kutokana na ushindi wa juzi walipoichapa Ndanda mabao 3-1.
“Hiyo inatupa morali zaidi ya kwenda kupambana kwa sababu sisi lengo letu ni kushinda mchezo huu kujihakikishia tunaifukuzia Simba katika nafasi ya juu,” alisema.
Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi jana jioni kuelekea mchezo huo na wachezaji wakiendelea kukaa kambini tokea ulipomalizika mtanange dhidi ya Ndanda, yote hiyo ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha inaibuka na pointi zote tatu.
Aidha itakumbukwa kuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex Septemba mwaka jana, timu hizo zilitoka suluhu.
Ushindi wowote wa Azam FC kwenye mchezo huo, utazidi kupunguza pengo la pointi baina yake na Simba na kufikia mbili na hivyo kuendeleza mapambano ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo, walioutwaa mara ya mwisho msimu wa 2013/2014.

No comments