KIUNGO WA YANGA AFUNGIWA MWAKA MMOJA

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, iliyokutana kwa siku mbili mfululizo Agosti 20 na 21, 2017, jijini Dar es Salaam, imepitia usajili wa majina ya klabu 40.

Katika idadi hiyo ya timu 40, kamati imepitia klabu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa mujibu wa katiba na kanuni za mashindano yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, inayoongozwa na Wakili Richard Sinamtwa, imegundua na kubaini kuwa mchezaji Pius Busita amesaini mikataba ya klabu mbili tofauti katika msimu mmoja wa 2017/18.

Kamati imebaini kwamba mchezaji huyo aliyechezea Mbao FC ya Mwanza msimu uliopita, amevunja Kanuni ya 66 ya Ligi Kuu ya Vodacom ambayo inaelekeza adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja. Mchezaji huyo amefungiwa kucheza mpira wa miguu kwa mwaka mmoja.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya  TFF, imebaini upungufu katika uwasilishaji wa majina ya wachezaji wa msimu wa 2017/18 kwa timu zote.

Klabu imeagiza klabu zote kuleta majina matatu ya wachezaji wasiopungua 18 na wasiozidi 30 wa kikosi cha timu ya vijana (U20).

Klabu zote zimeagizwa kuanisha wachezaji wa zamani na wapya na klabu wakakotoka kwa timu zote mbili za wakubwa na vijana.

Kamati imezitaka klabu hizo pia kuzingatia matakwa ya kanuni kwa kila mchezaji ambaye atapewa leseni ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi daraja la Kwanza.

Matakwa hayo ambayo ambayo yamesisitizwa ni kila mchezaji kujaziwa fomu ya utimamu wa mwili ‘Medical Form’ ya TFF.

Pia Klabu zinatakiwa kuwasilisha nakala tatu za mikataba (Contracts) ya kila mchezaji katika Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Uthibitisho wa kukatiwa Bima ‘Insurance’, Barua ya Uhamisho ‘Release Letter’ kutoka timu ambayo ametoka.

Kadhalika sharti jingine linahusu wachezaji wa kigeni ambako kila mchezaji hana budi kuwa na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na kulipwa Ada ya ushiriki ya msimu Sh. 2,000,000.

Klabu zimeagizwa kikamilisha utaratibu wa usajili kabla ya Agosti 24, 2017.

No comments