AZAM FC YABADILI MUUNDO WA UONGOZI

BODI ya Wakurugenzi ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya mabadiliko kwenye muundo wa uongozi wa klabu hiyo.
Mabadiliko hayo yaliyofanywa hivi karibuni yamehusisha nafasi ya Bodi hiyo, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti pamoja na kufuta cheo cha Meneja Mkuu na kukirejesha kile cha Ofisa Mtendaji Mkuu.
Akitangaza mabadiliko hayo mbele ya vyombo vya habari leo, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, alisema kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa timu hiyo, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’, sasa anaondoka kwenye nafasi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo.
Alisema kuwa bodi hiyo pia imemteua Shani Christoms kuwa Mwenyekiti mpya wa Azam FC, ambaye awali alikuwa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo.
Aidha kwa mujibu wa mabadiliko hayo, nafasi ya Christoms imezibwa na bodi hiyo kwa uteuzi wa Abdulkarim Mohamed Nurdin ‘Popat’, ambaye amewahi kuwa mchezaji wa timu hiyo wakati Azam FC ikiitwa Mzizima.
Mbali na kuichezea timu hiyo, pia amesomea mafunzo ya ukocha na mwanzoni mwa mwaka huu alisomea mafunzo ya uongozi wa soka.
Idd alimalizia kwa kusema katika kuboresha safu ya uongozi wa timu hiyo, bodi hiyo imemteua Abdul Mohamed, kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC na kukifuta cheo chake cha awali cha Meneja Mkuu.
Wengine wanaounda sekretarieti hiyo ya Azam FC, ni Meneja wa timu, Phillip Alando na Ofisa Habari, Jaffar Idd.

No comments