MALINZI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI NCHINI BRAZIL

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Shirikisho la Mpira Brazil (CBF), kutokana na vifo vya wachezaji wa timu ya soka Chapecoense Real ya Brazil.
Rais wa TFF Malinzi, katika salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Brazil (CBF), Lucca Victorelli  amesema ajali hiyo iliyoua watu wengi ni tukio la kusikitisha kwenye familia ya soka duniani na limetokea katika kipindi kigumu.
Rais Malinzi ambaye alituma salamu hizo pia kwa mashabiki wa Chapecoense na Jumuiya ya soka na wanafamilia wengine wa nchini Brazil, amesema: “Mawazo yetu yapo kwa wahanga wa ajali hiyo, familia na jamaa zao.”
Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri juzi Jumatatu kutoka Brazil kupitia Bolivia kwenda Colombia ilibeba abiria 81 wakiwamo wafanyakazi na wachezaji wa Chapecoense Real ya Brazil kabla ya kuanguka kwenye milima ya Colombia.
Wachezaji hao wa Chapecoense Real ya Brazil walikuwa wakisafiri kwenda kucheza mechi ya fainali ya michuano ya ubingwa wa Kombe la Amerika ya Kusini (Copa Sud Americana). Walikuwa ni miongoni mwa abiria 81.
Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Amerika ya Kusini, iliyotarajiwa kuchezwa leo Jumatano Novemba 30, 2016 ambako Chapecoense Real ingecheza dhidi ya Atletico Nacional ya Colombia.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba wachezaji wa timu ya Chapecoense Real ya Brazil, awali ilitoa taarifa ya hali ya hatari iliyosababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme, na hatimaye kuanguka muda mfupi baadaye karibu na mji wa Medelin.
Taarifa za vifo hivyo, zimethibitishwa na Mkuu wa Mamlaka ya Anga ya Brazil, Alfredo Bocanegra aliyesema walionusurika ni Watu watano wakiwamo wachezaji watatu wa Chapecoense na wafanyakazi wawili wa ndege hiyo.
Wachezaji walionusurika wanatajwa kuwa ni Alan Ruschel, golikipa Danilo na Jackson Follmann na kwamba walipatiwa huduma ya kwanza katika hospitali iliyoko katika mji wa Le Ceja nchini Colombia.

No comments