AZAM FC YATELEZA MABATINI,SASA VITANI NA NJOMBE MJI
HAIKUWA siku nzuri jana kwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
Awali mchezo huo ilikuwa ufanyike juzi Alhamisi kabla ya kuahirishwa kufuatia mvua kubwa kunyesha mkoani humo na maji mengi kutwama kwenye sehemu ya kuchezea uwanjani hapo.
Azam FC imepoteza mchezo huo ikiwa kwenye vita kubwa ya kuhakikisha inamaliza kwenye nafasi mbili za juu kwenye msimamo, ambapo kwa matokeo hayo imebakia katika nafasi ya tatu ikiwa nazo 45 ikizidiwa pointi 10 na kinara Simba yenye mchezo mmoja mkononi iliyofikisha 55.
Azam FC pamoja na kuonekana kupwaya kwenye eneo la ushambuliaji jana, pia kwa kiasi chake iliathiriwa na hali mbaya ya uwanja ambao hairuhusu kwa kiasi kikubwa kuonyesha ufundi.
Ruvu Shooting iliyojipatia bao moja katika kila kipindi cha mchezo huo, ilianza kutikisa nyavu za Azam FC dakika ya 28 kufuatia uzembe uliofanywa na kipa wa Azam FC, Razak Abalora, aliyeokoa vibaya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Khamis Mcha ‘Vialli’, uliojaa wavuni.
Adhabu hiyo ndogo ilitokana na kiungo Braison Raphael kumfanyia madhambi Abdulrahman Mussa, wakati akijaribu kumdhibiti pembeni kidogo ya eneo la 18.
Azam FC ililazimika kucheza pungufu dakika 16 za mwisho za mchezo huo kufuatia mwamuzi Shomari Lawi, kumuonyesha kadi nyekundu nahodha msaidizi wa timu hiyo, Agrey Moris, iliyotokana na kadi ya pili ya njano, hali iliyofanya nahodha Himid Mao ‘Ninja’ kumalizia dakika hizo akicheza kama beki wa kati sambamba na Abdallah Kheri.
Shooting ilitumia upungufu huo wa Azam FC kujipatia bao la pili dakika ya 80 lililofungwa na Fully Maganga, aliyevunja mtego wa kuotea kabla ya kukokota mpira na kufunga bao hilo.
Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kushuka tena dimbani kesho Jumapili kuvaana na Njombe Mji, mechi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.15 usiku.
Mchezo huo ni muhimu sana kwa Azam FC kwa ajili ya kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi, ambapo hivi sasa imebakisha mechi sita tu kumaliza msimu wa ligi.
Katika kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na timu hiyo, leo Jumamosi usiku kikosi cha Azam FC kitafanya mazoezi ya mwisho mwisho ili kujiweka vizuri na mchezo huo, ambao itaucheza baada ya saa 51 kupita tokea ichezea na Ruvu Shooting.
Timu hizo zilipokutana kwenye raundi ya kwanza mchezo uliopigwa Uwanja wa Sabasaba, Njombe, Azam FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Moris baada ya winga Enock Atta kuangushwa kwenye eneo la 18.
Wakati Azam FC ikitarajia kumkosa Moris atakayekuwa akitumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja kufuatia kadi nyekundu iliyotokana na kadi mbili za njano, mshambuliaji Shaaban Idd, aliyebanwa kifua mechi iliyopita na Mbeya City hadi kukimbizwa hospitali huenda akarejea baada ya kuruhusiwa kuanza mazoezi.
Wachezaji wengine watakaoendelea kukosekana ni mabeki David Mwantika, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, ambao ni wagonjwa huku mshambuliaji Wazir Junior, akiwa anatafuta ufiti baada ya kutoka kwenye majeraha ya kifundo cha mguu.
CHANZO; MTANDAO WA AZAM FC
Post a Comment