MAHAKAMA IMEUTAKA UPANDE WA MASHTAKA KUWA WAKWELI KWENYE KESI INAYOWAHUSU VIONGOZI WA SIMBA

Na Unique Maringo
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka kuwa wakweli  katika kesi 
ya kutakatisha fedha na kugushi inayomkabili Rais wa  Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange `Kaburu`.

Wakili wa serikali Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Victoria Nongwa alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba kuna nyaraka zinamaliziwa kufanyiwa kazi.

Wakili upande wa utetezi Philemon Mtakyamirwa alidai kuwa ni mara ya tatu upande wa mashtaka kudai kuwa wanamalizia upelelezi hivyo aliomba tarehe ya karibu.

Hakimu Ngongwa aliutaka upande wa mashtaka wajitahidi kuwa wakweli na kukamilisha upelelezi.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 18 mwaka huu kwaajili ya kutanjwa.

Evans Elieza  Aveva na makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani 300,000.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa  walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Machi 15,2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala Aveva akijua alitoa nyaraka za uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakati akijua ni kosa.

Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,2016 Dar es Salaam  kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha,Aveva anadaiwa kuwa kati ya Machi 15,2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa  Machi 15,2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni alimsaidiaAveva  kujipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.

Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

No comments