HERNANDEZ AFURAHISHWA NA VIWANGO VYA WACHEZAJI
KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa amefurahishwa na
viwango vya baadhi ya nyota waliokuja kufanya majaribio ya kujiunga na timu
hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa leo.
Azam FC
jana usiku ilimaliza programu ya kukifanyia tathimini kikosi chake kwa kuichapa
Ruvu Shooting mabao 3-1 kwenye mchezo wa kujipima ubavu, ambao pia iliutumia
kuwapima wachezaji tisa waliokuja kwa majaribio, mabeki wa kati Nkot Mandeng
Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec Mimosa, Ivory
Coast).
Kiungo
mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport Garoua, Cameroon), Abdallah Khamis
pamoja na washambuliaji Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon), Samuel
Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana), Konan Oussou
(Tala’ea El-Gaish SC, Misri) na Jean Karekezi.
Mabao
mawili kati ya matatu ya Azam FC usiku wa jana yalifungwa na nyota waliokuwa
majaribio, ambao ni Ofori aliyefunga la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi safi
ya Gadiel Michael na Afful akitumia juhudi binafsi kwa kumzidi maarifa beki
pemmbeni ya uwanja na kupiga shuti kali lililojaa wavuni.
Hernandez
ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa muda kuanzia sasa anatarajia
kupeleka mapendekezo yake kwa uongozi wa timu hiyo juu ni nyota gani kati ya
hao wasajiliwe, huku akidai kwa viwango alivyoviona anaamini ya kuwa wachezaji
watakaosajiliwa wataweza kuisaidia sana Azam FC.
“Raundi
ya kwanza imemalizika na tumeona mapungufu ambayo tunataka kuyarekebisha kwa
ajili ya raundi ya pili na ndio maana tumejaribu kutafuta wachezaji ambao
tunahisi wanaweza kutusaidia kwenye timu raundi ya pili na michuano mingine,
kilichobakia sasa hivi tunaamini ya kwamba baadhi ya wachezaji ambao
wameonekana wanafaa kabisa kusaidia kwenye timu yetu,” alisema.
Kocha
huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema anaamini ya kuwa kikosi
chake kikiingia raundi ya pili kitaweza kupambana ipasavyo basi matokeo
yatakuwa mazuri na hatimaye kuweza kufikia nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo
kuliko nafasi ya tatu ambayo timu hiyo inashika hivi sasa ikiwa na pointi 25
pungufu ya pointi 10 na kinara Simba aliyejikusanyia 35 huku Yanga akiwa nazo
33 (nafasi ya pili).
“Hapa
hatukuja kwa ajili ya starehe tumekuja kikazi, tunaamini nafasi ambayo tunayo
tunapointi nyingi ambazo tunatakiwa kuzikamilisha ili kuweza kuwafikia hao
ambao wapo juu Simba na Yanga, tumejua makosa yetu tuliyofanya raundi ya kwanza
na ndio haya tunayafanyia kazi hivi sasa ili kuweza kuyakamilisha, ili hatimaye
tuweze kufanya vizuri na hatimaye kuchukua ubingwa, kwa hiyo ni muda ambao
tunajiandaa kwa kuziba mapengo ambayo yapo na kuweza kuingia kwenye ushindani
zaidi,” alimalizia.
Mara baada ya mchezo wa jana dhidi ya Ruvu Shooting, benchi la
ufundi la Azam FC limewapa mapumziko ya wiki mbili wachezaji wa kikosi hicho
kabla ya kuanza tena mazoezi Desemba 3 mwaka huu kwa ajili ya kuanza maandalizi
ya mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup)
na michuano ya Kimataifa.
Post a Comment