KILIMANJARO QUEENS NEEMA TUPUKILIMANJARO QUEENS NEEMA TUPU
Ubingwa Kombe la CECAFA Chalenji kwa timu za mpira wa miguu za wanawake katika nchi za Afrika Mashariki, umewavutia wadau wengi kwa kiwango kikubwa hivyo kushusha neema kwa wachezaji hao wa timu ya taifa ya Tanzania Bara maarufu kama Kilimanjaro Queens ambayo imeandika historia ya kutwaa taji hilo ikiwa ni taifa la kwanza katika mashindano hayo mapya.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amefurahishwa na ubingwa wa timu hiyo akisema: “Si ubingwa tu, bali umefuta dhana ya Wakenya ambao siku zote wamekuwa wakitangaza Mlima Kilimanjaro uko kwao Kenya wakati upo hapa Tanzania. Kwa kuifunga Kenya, mmefanya kazi nzuri.”
Kutokana na ubingwa huo na kuitetea nchi, Nape ambaye aliongozana na Wabunge sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliahidi kuitafutia timu hiyo ya taifa ya wanawake mdhamini na kwa baadhi ya wachezaji kupata ajira sehemu mbalimbali hususani kwa makampuni kadhaa ambayo yamewekeza hapa nchini.
“Niko na Wabunge hapa. Bunge la Novemba ambalo litaanza Novemba mosi, naawaalika bungeni. Tutazungumza na Spika ili kuvunja kanuni za bunge iloi ninyi muingie bungeni la kombe letu. Nitawaomba wabunge wakate posho zao kidogo, ili kuwazawadia ninyi pale mtakapofika. Tutakuwa na mchezo wa mpira wa miguu kati yenu na wabunge, na kila bao moja mtakalowafunga wabunge, litalipiwa Sh milioni moja.”
“Mimi ndiye nitakayehesabu mabao, lakini mkae mkijua haitakuwa kazi rahisi kuwafunga wabunge. Wako vizuri,” alisema Nape ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama na kauli yake hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, William Ngeleja aliyeambatana wabunge wengine akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, Esther Matiko.
Wengine waliokuwako ni Bupe Mwakang’ata, Alex Gashaza, John Kanuti ambaye mbali ya ubunge pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kadhalika Venance Mwamoto – nyota wa zamani wa timu ya Taifa na Kocha wa daraja B.
Kwa upande wa TFF, Rais wa Shirikisho la Miguu Tanzania, Jamal Malinzi alitoa ahadi ya Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh milioni 22) kwa timu hiyo baada ya kutwa taji hilo kabla ya timu hiyo leo kutembelea Kampuni ya Airtel ambako Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel-Tanzania, Beatrice Singano akatangaza kampuni yake kuendelea kudhamnini mashindano ya kuibuka vipaji ambavyo vimekuwa vikiitoa Tanzania kimasomaso katika mashindano ya kimataifa.
Kati ya nyota 20 wa Kilimanjaro Queens waliotwaa taji hilo, wanane walipitia mashindano ya Airtel kwa miaka tofauti katika udhamini ambao kwa mwaka huu ilikuwa ni mara ya sita kwa kampuni hiyo inayofanya vema kwenye soko la huduma za simu, kudhamini mashindano ya Airtel Rising Stars (ARS).
Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-0 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Post a Comment