AZAM FC YAITUPA YANGA NAFASI YA TATU

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemaliza katika nafasi ya pili kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Yanga mabao 3-1.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa usiku wa kuamkia leo, ulikuwa mkali na wa aina yake kwa timu zote kuonyeshana ushindani lakini Azam FC ikionekana kutengeneza nafasi nyingi za mabao.

Mabao ya ushindi ya Azam FC yamewekwa kimiani na Yahya Zayd aliyefunga la kwanza kwa staili ya ‘outer’ dakika ya nne tu akiunganisha pasi ya Shaaban Idd, bao lililodumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.

Yanga ilisawazisha bao hilo dakika ya 49 baada ya beki wa Azam FC, Abdallah Kheri, kujifunga kwa kichwa kwa bahati mbaya wakati alipokuwa kwenye harakati za kuokoa krosi iliyochongwa na beki wa kulia wa Yanga, Ramadhan Kessy.

Azam FC iliyomaliza nafasi ya nne msimu uliopita kwenye ligi hiyo, iliendeleza mashambulizi ya kasi langoni mwa Yanga, na alikuwa ni Shaaban, aliyeipeleka mbele tena timu yake kwa bao safi la pili dakika ya 59 akiunganisha krosi ya winga Idd Kipagwile, kwa staili ya ‘overhead kick’.

Hilo ni bao la tisa kwa Shaaban msimu huu wa VPL na la 10 kwenye michuano yote, Azam FC iliendeleza kasi na dakika ya 67 kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, alitumia vema krosi ya Zayd na kuipatia bao la tatu kwa shuti.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kumaliza msimu na pointi 58, ikiizidi Yanga pointi sita iliyosaliwa nazo 52 katika nafasi ya tatu huku Simba imetwaa ubingwa kwa pointi zake 69.

Wakati pazia la ligi likifungwa, jumla ya timu mbili zimeshuka daraja ambazo ni Majimaji na Njombe Mji, ambapo timu sita zimeshapanda daraja, African Lyon, KMC, JKT Tanzania, Coastal Union ya Tanga, Alliance Schools ya Mwanza na Biashara United ya Mara zinazokamilisha idadi ya timu 20 za msimu ujao.

Source,mtandao wa Azam FC.

No comments