LICHA YA USHINDI WA 3-2 SINGIDA WALALAMIKIA TATIZO HILI

Na Said Ally,Unguja
Kocha msaidizi wa timu ya Singida United Jumanne Charle amesema kwamba licha ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Zimamoto lakini hali ya hewa katika mchezo huo wa kombe la mapinduzi imewapa wakati mgumu wachezaji wake.

Charle alisema kwamba  wachezaji wake walionekana kuchoka kutokana na uchovu mwingi wa safari ya kutoka Njombe walipokwenda kushiriki mchezo wa ligi kuu ya Tanzania bara na pia kucheza kwenye jua kali huku uwanja ukiwa na nyasi bandia umewapa wakati mgumu zaidi .

Alisema kwamba tatizo lingine ambalo lilipelekea kuruhusu magoli mawili  kwenye pambano hilo ni kutokana na kukosa umakini kwa walinzi na golikipa ambao walikuwa hawana mawasiliano mazuri ya kuokoa mipira iliyoelekezwa langoni.

Aidha alisema kwamba ushindi huo unawapa chachu ya kucheza kwa juhudi zaidi katika michezo mingine ili kikosi hicho kifanikiwe kuwa mabingwa wa kombe la Mapinduzi kwa msimu huu.

Singida United ilijipatia ushindi huo wa magoli 3-2 kupitia kwa wachezaji wake,Deusi Kaseke dk 7,Danny Usengimana dk ya 21 huku goli la tatu likifungwa na Kigi Makasi kunako dk ya 84 ya mchezo.

No comments