KOCHA MLANDEGE ASIKITISHWA NA KAMATI YA MASHINDANO YA MAPINDUZI
Na,Said Ally,Zanzibar
Kocha wa timu ya Mlandege Abdul-Hamin Rashidi amesema kwamba sababu ambayo imewaondosha katika michuano ya kombe la Mapinduzi ni ukosefu wa umakini kwa wachezaji wake.
Rashidi ameyasema hayo baada ya leo hii kikosi hicho cha Malandege kukubali kipigo cha jumla ya magoli 3-0 mbele ya Singida United inayoongoza katika msimamo wa kundi B ikiwa na alama 9.
Alisema kwamba wachezaji wameshindwa kuwa na umoja kwani kila mchezaji amecheza kivyake vyake tofauti na maelekezo ambayo aliwapatia kabla ya mchezo.
Aidha katika hatua nyingine Rashidi alisema kwamba kamati ya mashindano ya kombe la Mapinduzi imeshindwa kutenda usawa kwa timu za Zanzibar hasa kwenye fedha ya kujikimu,usafiri na maswala mengine ya uendeshaji wa timu katika michuano hiyo.
"Mashindano ni mazuri lakini kuna utofauti kidogo,timu za kwetu kama azipewi kipaumbele katika haya mashindano,kwa sababu wenzetu wanapewa pesa za kujikimu,usafiri na hoteli lakini sisi kila kitu tunajitegemea wenyewe"alisema Rashidi.
Hata hivyo aliongeza kwa kusema kwamba endapo kamati kama itashindwa kubadilika anaamini timu za Zanzibar zinaendelea kufanya vibaya katika michuano hiyo kwani vilabu vingi havina udhamini na kamati husika inashindwa kuleta usawa kwenye mashindano hayo kwa kuzipa kipaumbele timu ngeni.
Post a Comment