YANGA YATUPWA NJE MICHUANO YA SPORTPESA

Timu ya soka ya AFC Leopard ya nchini Kenya imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali katika michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuwaondosha mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania bara,timu ya Yanga kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-2.

Mchezo huo ulimalizika kwa dakika 90 kwa timu hizo kushindwa kufungana hivyo kuamuliwa kwa mikwaju ya penati iliyowafanya Yanga kukosa penati mbili ambazo ziliokolewa na mlinda mlango wa timu ya AFC Leopard Jan Otieno.

Mchezaji Said Mussa kutoka timu B na Said Makapu ndio wamekosa mikwaju ya penati iliyowafanya kuwapa nafasi wapinzani wao kufuzu kwenye hatua ya fainali.

Baada ya mchezo huo kukamilika,kocha msaidizi wa AFC Leopard Denis Kitambi alisema kwamba amefurahishwa na matokeo hayo kwani ilikuwa kazi ngumu kuitoa timu mwenyeji ambayo pia ni bora na yenye mashabiki wengi.

Kitambi alisema kwamba kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa fainali itakayopigwa siku ya jumapili ambapo anaamini watafanikiwa kuwa mabingwa wa michuano hiyo.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa timu ya Yanga Juma Mwambusi alisema kwamba kupitia mashindano haya yamewapa picha ambayo itawasaidia namna ya kukifanyia marekebisho kikosi hicho huku akidai kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa timu hiyo watapandishwa katika timu ya wakubwa.

Aidha Mwambusi ametoa ushauri kwa waandaji wa michuano hiyo kuwa ni vyema wakati mwingine wakapanga muda mzuri wa kuchezwa kwa mashindano hayo ili timu zote ziwe na wachezaji kamili tofauti na ilivyokuwa kwa msimu huu.

Kuondoshwa kwa Yanga kwenye michuano hiyo ya SportPesa kumeendelea kuleta jinamizi kwa timu za Tanzania ambazo zimeshiriki michuano hiyo baada ya timu zote nne kutolewa na vilabu vya Kenya.

No comments