TAIFA STARS IPO KAMILI KUWAVAA LETHOTO

Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars,Salum Mayanga amesema kwamba kikosi chake kimejiandaa vyema kuwakabili Lethoto hapo kesho katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika, mchezo unaotarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.

Mayanga alisema kwamba hali ya wachezaji kiujumla wako vizuri na kila mmoja ana hamasa ya kufanya vizuri kwenye pambano hilo ambalo linataraji kuwa na ushindani wa hali ya juu kwa pande zote.

"Maandalizi tuliyofanya tangu tulipoanza kambi kiukweli ni mazuri ambayo yananipa matumaini kwa kikosi chetu kuibuka na ushindi,nafahamu wapinzani wetu ni wazuri na nilishuhudia mechi zao mbili walizocheza ambapo nilifahamu mbinu zao"alisema Mayanga.

Aidha Mayanga amewataka mashabiki wa soka hapa nchini kujitokeza kwa wingi hapo kesho ili kuwapa sapoti ambayo itawafanya wachezaji wacheze kwa kujituma zaidi.

Kwa upande wake nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samata alisema kwamba kwa upande wao kama wachezaji wanaingia kwenye pambano hilo wakifahamu umuhimu wa mchezo huo hivyo watahakikisha watacheza kwa juhudi kubwa na kufanikiwa kuibuka na ushindi.

No comments