WENGER AKUBALI KUBAKI ARSENAL

Kocha wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekubali kutia saini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu hiyo mkataba unaomfanya aendelee kusalia kwenye timu hiyo kwa zaidi ya miaka 21 ambayo amedumu na washika bunduki hao.

Kocha Wenger na mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke walikutana hapo jana kujadili mustakabali wa kocha huyu Mfaransa, uamuzi ambao uliwasilishwa pia kwenye kikao cha bodi ya klabu ya Arsenal Jumenne asubuhi.
Klabu ya Arsenal sasa inatarajia kuweka wazi makubaliano haya kwa uma Jumatano ya wiki hii.
The Gunners walimaliza kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa jedwali la ligi kuu ya England msimu huu, ikiwa ni mara ya kwanza kumaliza nje ya nafasi nne za juu toka kocha huyo alipochukua jukumu la kukinoa kikosi hicho mwaka 1996.
Arsenal imemaliza kwa alama 18 nyuma ya machampioni wa ligi hiyo klabu ya Chelsea, lakini wakawafunga mabingwa hawa kwenye mchezo wa fainali ya FA Cup Jumamosi iliyopita.
Mkataba wa kocha Arsene Wenger ulikuwa unatamatika mwishoni mwa msimu huu.
Kocha huyu ameiongoza timu yake kutwaa mataji matatu ya ligi kuu na mataji menne ya FA katika misimu tisa ya mwanzo aliyoichukua timu hiyo.
Mwaka 2003 na 2004, alikuwa kocha wa kwanza toka mwaka 1888 na 1889 kuongoza timu yake kumaliza msimu bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Lakini baada ya kushinda taji la FA mwaka 2005, iliwabidi wasubiri miaka tisa baadae kushinda taji jingine, na lilikuja baada ya kuwafunga Hull City mwaka 2014 kuchukua taji la FA kabla ya kushinda taji hilo mwaka uliofuata.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal wameonesha kutokuwa na furaha na kocha Wenger wakimlaumu kwa matokeo mabaya ya msimu huu pamoja na kufungwa jumla ya mabao 10-2 na klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya Machi 16 mwaka huu.
Arsenal ilimaliza kwa kushinda mechi tano mfululizo lakini haikutosha kuwabeba kumaliza juu ya klabu ya Liverpool kuchukua nafasi ya 4 ambayo ingewawezesha kushiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya.

No comments