MBOWE ASEMA JESHI LA POLISI LILIFANYA MAAMUZI YA HARAKA YA UPIGAJI MABOMU KATIKA UWANJA WA TAIFA


Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo [CHADEMA] Freeman Mbowe amesikitishwa na hatua iliyochukuliwa na mashabiki wa Simba ya kung'oa viti uwanjani wakati wa pambano la watani wa jadi  Simba na Yanga mechi iliyomalizika kwa timu hizo kufungana kwa bao 1-1.

Mbowe ameyasema hayo wakati akiongea na mtangaziji na mmiliki wa kituo cha ABM RADIO ya mkoani Dodoma Abdalah Majura,ambapo amesema kwamba kitendo hicho cha kung'oa viti ni kitendo cha aibu kwa Taifa wala sio kwa klabu ya Simba pekee kwani michezo ni furaha kwa watu wote.

Mbowe amesema kwamba mashabiki wa Simba walipaswa kuwa watulivu bila ya kujali kua goli si halali ama ni halali kwa sababu mwamuzi ndie anaetafasiri sheria 17 za soka hivyo ni vyema wangekaa kimya kwa utulivu ili baadae vyombo husika vichukue jukumu lake kama kungekuwepo na malalamiko.

Aidha amesema kwamba pia Jeshi la Polisi lilipaswa kutumia njia mbadala ya kuzuia vurugu kwa upande wa mashabiki wa Simba kwani waliwahi kurusha mabomu katikati ya jukwa la Simba na pia mabomu hayo pia yalilenga sehemu ambayo mashabiki walikua hawafanyi vurugu yeyote.

"Mi nadhani Polisi hawakutenda haki katika upigaji Mabomu kwani kama kule juu mashabiki walikua wametulia wamekua hawafanyi vurugu lakini nashangaa hayo mabomu yalielekezwa kwao na pia kuwai kupiga mabomu kulileta hofu ya pambano husika hivyo ni vyema hili jambo kwa Polisi likaangaliwa kwa umakini ili siku nyingine yasitokee mambo kama haya"alisema Mbowe.

Mbali na hilo pia Mbowe amesema kwamba ni vyema wamiliki wa uwanja wa Taifa wakafanya matengenezo sahihi ya utengenezaji wa viti kwani inaonekana viti havikiwa imara katika sehemu hiyo.

"Hili ni jambo pana sana unaweza kujiuliza inakuaji viti ambavyo vimekabarabatiwa vizuri alafu mtu anaweza kung'oa viti tena pasipo kutumia nguvu yeyote na hii si mara ya kwanza swala hili la ung'oaji wa viti, sasa umefika wakati wa wahusika kujitafakali na zaidi kuboresha miundo mbinu ya uwanja huo ambao ni rasmali ya nchi"alisema Mbowe.

Hata hivyo Mbowe hakusita kuweka mapenzi yake hadharani kwa kusema yeye ni mmoja wa mashabiki wa Yanga wa muda mrefu ingawa hapendi kuonekana michezoni lakini amesema kwamba ushabiki wake wa Yanga hauwezi kumfanya ashindwe kuona haki inatendeka kwa upande wa Simba kama wanastahili kupata haki kwa kile walichokifanya.

No comments