MBEYA CITY YAKUSANYA POINTI TATU NYUMBANI
Bao la dakika ya 27 kipindi cha kwanza lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa kati Ditram Nchimbi, lilitosha kuhitimisha dakika 90 za mchezo namba 50 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliozikutanisha Mbeya City fc dhidi ya wageni Mwadui Fc kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya matokeo yaliyomuacha kocha wa Mwadui Fc akitangaza kujiuzuru kufundisha pia kujihusisha na mchezo wa soka hapa nchini.
Kwenye mchezo huo uliokuwa na kasi ya aina yake, timu zote zilianza dakika 45 za kwanza kwa nguvu kubwa iliyoacha mashambilizi ya kila mara pande zote mbili lakini uimara wa walinda milango, Owen Chaima na Shaban Kado ulifanya washambuliaji wa timu zote kushindwa kufunga mabao ya mapema.
Dakika ya 27, mpira ulioanzia upande wa kulia kwa John Kabanda aliyefanikiwa kuupitisha vizuri katikati ya uwanja kwa nahodha Kenny Ally, ulifanikiwa kufika kwenye miguu ya Ditram Nchimbi ambaye akiwa nje kidogo ya eneo la 18 la Mwadui Fc alifumua shuti kali lililomshinda kipa Kado na kutinga wavuni moja kwa moja,kuandika bao la kwanza kwa City lililodumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, kocha wa City Kinnah Phiri alifanya mabadiliko kwa kumtoa, Joseph Mahundi na nafasi yake kuchukuliwa na Hamidu Mohamed pia alimtoa Omary Ramadhani na kuingia Salvatory Nkulula huku Rajab Zahir aliyepata majeraha akimpisha Ramadhani Chombo, mabadilliko yaliisaidia timu yake kuimarisha safu ya kiungo na hatimaye kufanikiwa kukamilisha dakika 90 matokeo yakibaki kama yalivyokuwa.
Post a Comment