AZAM FC WAKO TAYARI KUIFUNGA SINGIDA UNITED

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejidhatiti vilivyo kuibuka na ushindi kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Singida United.
Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi hii saa 1.00 usiku, unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na ubora wa timu zote mbili na pia zikikaribiana kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Wakati Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 35, Singida United inafuatia nafasi ya nne ikiwa nazo 34, huku timu mbili za juu Simba ikiwa kileleni kwa pointi 42 na Yanga yenye kiporo mchezo mmoja imejikusanyia 37 katika nafasi ya pili.
Kauli za kujihakikishia ushindi zimetolewa na Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche na kiungo Frank Domayo.
"Tunamshukuru Mungu wachezaji wote wako vizuri na wana hali ya mchezo kwa sababu tunaangalia kwenye mazoezi wamefika kwa muda na wanaanza wenyewe taratibu kabla hatujawaandalia programu hii inatupa moyo sana kiasi kwamba kuona jinsi gani walivyokuwa na hamu ya ushindi.
“Nafikiri tuko vizuri tunaangalia michezo iliyopita, matatizo tuliyokuwa nayo kwenye michezo iliyopita tunajaribu kuyasawazisha yasijirudie katika mchezo ujao halafu tunaiangalia Singida jinsi gani ilivyo ina uzuri gani ina udhaifu gani ili tutumie madhaifu yao na mazuri yao tuweze kuyadhibiti,” alisema Cheche.
Aliongeza kuwa: “Tahadhari lazima tuingie nayo iwe nafasi yoyote uliyokuwepo lakini lazima tuingie na tahadhari kwa sababu hatutaki kufungwa tunataka kushinda kwanza tunaweka usalama katika ulinzi wetu tuhakikishe mpira hauingii kwenye nyavu zetu halafu tutengeneze mipango ya kuhakikisha tunapata magoli ambayo yatatupa ushindi na pointi tatu ili tuzidi kuwavuka zaidi hao wapinzani wetu.”
Naye Domayo aliyekuwa na kiwango bora kabisa kwenye mchezo uliopita dhidi ya KMC, alisema kuwa wao kama wachezaji watapambana kadiri ya uwezo wao ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi kutokana na umuhimu wa mtanange huo.
“Tutapambana na tufafuata maelekezo ya kocha, tutajituma kwa nguvu zetu zote ili tuweze kuibuka na ushindi katika mechi hiyo muhimu, mashabiki wa Azam FC naweza kuwaambia kuwa watuombee kwa sababu ligi bado ngumu kila timu inajitahidi kadiri ya uwezo wao ili iweze kuibuka na ushindi.
“Watuombee, waje kutushangilia kwa sababu mashabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani kwa hiyo naweza kusema waje kwa wingi washangilie timu na sisi hatutaweza kuwaangusha,” alisema Domayo.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 mchezo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, bao la Azam FC ilikifungwa na Paul Peter huku Singida wakitangulia kutupia kupitia kwa Danny Usengimana.

No comments