MWAMBUSI AWAPONGEZA WACHEZAJI KWA KUWAADABISHA ASHANTI UNITED

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Yanga,Juma Mwambusi amewapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa jumla ya bao 4-1 mbele ya wauza mitumba Ashanti Uniteda katika mchezo wa kombe la FA uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Mwambusi amesema kwamba wachezaji wake kwa kiasi kikubwa wamecheza vizuri kwa jinsi ya maandalizi waliyoyafanya kuelekea kwenye mechi hii ambapo amedai kuwa hawakuwa na maandalizi ya kutosha.

Amesema kwamba mechi ya leo ilikuwa lazima washinde kwani ndiyo mabingwa watetezi wa kombe hilo,hivyo kwa matokeo waliyoyapata ni mazuri kwao na sasa wanajipanga na timu nyingine watakayopangiwa nayo kwenye hatua nyingine.

"Ukweli wachezaji hawakucheza kile kiwango kinachotakiwa kwani unaweza kuona hata namna jinsi walivyokuwa wanapokea mipira lakini nadhani walimu tumeyaona mapungufu tutaenda kuyafanyia kazi"alisema Mwambusi.

Katika hatua nyingine Mwambusi ameweka bayana sababu za kuendelea kumtumia mchezaji Osca Joshua kwenye namba tofauti na ile iliyozoeleka ambapo mara nyingi amekuwa akimudu namba tatu.

Mwambusi amesema kwamba Osca si mara ya kwanza hii leo kucheza namba tofauti,hivyo ni mipango yao ya kuona mchezaji ana mudu kucheza namba nyingi kwa ajili ya kuisadia timu inapokuwa kwenye wakati mgumu hususani mchezaji anapopata kadi nyekundu.


No comments