ASHANTI MBIONI KUIKABILI YANGA PASIPO MAANDALIZI

Kocha mkuu wa timu ya Ashanti United ya jijini Dar es salam,Maalim Salehe amesema kwamba shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini limeendelea kushindwa kuendesha kwa weledi mpira wa miguu hapa nchini akidai kuwa kwa mara nyingine wameshindwa kutenda haki katika utoaji wa ratiba ya michezo ya kombe la FA.

Salehe amesema kwamba kama kocha mkuu wa timu ya Ashanti anashangaa kuona ratiba yao inaonyesha kuwa siku ya kesho wanacheza na Yanga mechi ya FA pasipo mpangilio mzuri wa utoaji wa taarifa kwa wahusika.

Amesema kwamba kwa upande wake tayari kwa siku ya jana alishawapa mapumziko mafupi wachezaji wake kwani alikuwa hafahamu kama siku ya kesho watakuwa na mechi tena ikiwakutanisha na timu kongwe hapa nchini.

"Ndugu mwandishi mimi taarifa za mechi nimepata leo asubuhi,hapo hapo jana niliwapa mapumziko wachezaji wangu maana nimeona ni vyema baada ya mazoezi magumu niwape mapumziko mafupi sasa kwa sasa sina jinsi itabidi tupeane taarifa turejee wote kambini"alisema Maalim Salehe.

Hata hivyo amedai kuwa ingawa ratiba hiyo si rafiki kwao lakini hapo kesho wanataraji kushika dimbani kucheza mchezo huo unaotaraji kupigwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kuanzia mishale ya saa kumi kamili jioni.

No comments